Nimeanguka kimapenzi na mtu nisiyemjua




Ndugu zangu mnaweza kushangaa ama kuhisi nimepungukiwa na akili kama nikiwasimulia kisa hiki kilichomkuta rafiki yangu wa karibu. Yeye ametokea kupendana na msichana baada ya kuchat nae kwenye simu na hadi dakika hii anafanya mpango wa kumuoa. Shida ni moja tu kuwa mawasiliano ni kwenye simu tu na hawana njia nyingine ya kuonana. Hii inamaana kuwa kama mmoja hana simu hata kwa mwezi basi hakuna njia ya kuwasiliana si kwa marafiki wala ndugu. kisa kilianza hivi:

Miezi sita iliyopita karimu alipokea ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa mtu asiyemjua ukisema "Hi dear, I miss you". Haikuwa ni mara yake ya kwanza kupokea ujumbe wa namna hii na mara nyingi huwa hajishughulishi kujibu wala kushtushwa na sms za namna hiyo. Hata hivyo alijikuta akiuhifadhi ujumbe huo bila sababu. Simu ya karimu mara huwa bize na hupokea sms nyingi kwa siku. Hivyo wakati mwingine hulazimika kuzifuta ili kutoa nafasi kwa sms zingine kuingia. Pamoja na utaratibu huo hakuwahi hata siku moja kufikiria kuifuta ile sms.

Ilimchukua mwezi mmoja na nusu bila kufanya jambo lolote na ile sms, hakuijibu wala kuifuta sms ile ya ajabu.

Fuatilia kisa hiki na upate kujua..karimu atachukua hatua gani baada ya kukaa na sms ile kwa takribani miezi miwili bila kumtafuta mhusika.....wiki ijayo hapa hapa JF

............................Mpya...........................Mpya................Mpya....................

Kijana Karimu anakutana na sms yenye utata na anaumua kufuatilia undani wa sms hiyo na mwisho wa siku anajikuta kwenye dimbwi zito la mahaba na mtu asiyemjua huku akipitia vikwazo vingi kutoka kwenye familia ya mpenzi wake. Je nini hatma yao wawili hao ambao wampendana bila kujuana sura wala umbo.

katika simulizi iliyopita tulipata kuona namna Karimu alivyoamua kumsaka mhusika aliyemtumia ujumbe ule wa mapenzi kwa kumpigia simu...tuendelee.

Sauti ya upande ilimshtua kidogo karimu kwa kuwa alihisi kama si ngeni masikioni pake. Akatulia akijaribu kuvuta kumbukumbu wapi aliwahi kusikia sauti hiyo bila mafanikio. Ndipo aliamua kuendelea na mazungumzo. Wakati huo wote alikuwa na uhakika na salio kwani alijiunga na mtandao maarufu kwa huduma ya extreme hivyo hakuwa na haraka ya kuishiwa salio.

Sauti: (kwa ukali) wewe nani na upataje namba yangu?

Karimu alijitutumua na kuendelea kumbana na maswali. "Utaniulizaje mi nani wakati wewe ndo ulienitumia sms, kwanza unaitwa nani na uko wapi?" sauti ile ilipoona karimu anakuja juu ilitulia na kurejea katika hali yake ya kawaida na kujitambulisha

Sauti: Mi naitwa nasma. niko unguja, mbona mi sijawahi kukutumia sms! alijibu kwa mshangao.

Karimu: "Sasa kama hukuwahi kunitumia sms hii ni ya nani au nikuforwardie uone ulituma lini na saa ngapi? Kuwa makini unapotumia simu sio mnasumbua watu nyie ndo mnaovunja ndoa za watu kwa papara zenu." alimaliza na kukata simu.

Pamoja na ukweli kuwa karimu alikata ile simu bado rohoni aliamini kuna jambo kwenye sauti ya nasma. Hiyo ilikuwa asubuhi jumatano ya tarehe 7 wiki moja tu baada ya kuona mwaka mpya.

Baada ya nusu saa ya mazungumzo yale alipokea sms kwenye simu yake na alipofungua alishtuka kuona imetoka kwa nasma. Iliandikwa hivi, "Nimeenda kwenye kabati langu na kuangalia notebuk ya mdogo nimekuta amesave namba hii kama mbongo, hivyo inawezekana ni yeye alikutumia sms hiyo" nilijikuta natabasamu bila sababu.

akamjibu kwa jeuri, "Basi mi nataka kuongea na huyo aliyenitumia sms, akifika mwambie anitext au aniflash". Nae akajibu "poa" akionyesha kutoridhika na jibu alilopata toka kwa karimu. Hadi dakika hiyo bado alikuwa na hisia za kuitambua sauti ile.

Kwa faida ya wafuatiliaji wa kisa hiki, Karimu ni kijana mwenye umri kati ya 25 na 30, anajishugulisha na uandaaji wa vipindi vya Redio na Tv na mara nyingi husafiri sehemu mbalimbali za Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa shughuli hiyo, hivyo aliamini inawezekana aliwahi kukutana na sauti ile wakati alipokuwa zanzibar ingawa hakuwa na uhakika.

Basi, karimu baada ya kumalizana na nasma aliendelee na shughuli zake huku kichwani sauti ya nasma ikijirudiarudia. Ilikuwa majira ya saa kumi na moja jioni ilipoingia sms kutoka kwa nasma, "Haya aliyekutumia sms huyo hapa chat nae, bye" ilimaliza sms hiyo.

Alipatwa na wasiwasi kidogo kwani alihisi nasma anataka kumghiribu hivyo akaamua kupiga badala ya kuchat nae. Basi mtoto wa kiume akaenda hewani, brrr brrr brrr brrr, simu ikaita na upande wa pili ikapokea, "Hello, Assalaam aleykum" akajibu Aleykum assalaam, naongea na nani? Ikajibu upande wa pili, mi naitwa raisa. Akaendelea kuuliza, wewe ndo uliyenitumia sms? Ikajibu ndio. Karimu akaishiwa na maneno.

Baada ya kimya kifupi karimu akachokoza, "Sasa raisa wewe umesema unanimiss kivipi wakati hata hunijui kwanza umepata namba yangu?" Raisa akajibu kwa utulivu, nimeitoa kwenye kipindi chako. Hapo mchezo ukaisha akabaki mdomo wazi kwa mshangao. Raisa akaendelea, "unajua karimu mi nakupenda na nimekuwa nikifuatilia kwa muda mrefu vipindi vyako". Hapo uzalendo ukamshinda Karimu akahoji, "Utanipendaje wakati hunijui wala sikujui huoni unataka kunizingua?" Raisa akaendelea kung'ang'ania na msimamo wake. Karimu alishindwa cha kusema zaidi ya kucheka.

Baada ya mazungumzo ya dakika kama 15 hivi, Raisa akaomba waongee usiku kwa kuwa dada yake (nasma) amekasirika sana ametumia simu yake kuwasiliana na wanaume na matokeo yake yeye anatukanwa bila sababu hivyo amelala kichwa kinamuuma sana. Akaendelea, "dada ni mkali sana na hapendi wanaume kwani anamashetani kichwani na wanaume wengi wamemtaka amewakatimua". Karimu hakushtuka sana kwani alijua kwa maneno yale lazima angekasirika tu. Pia aliona ahueni kwani muda wa extreme ulikuwa unaelekea kuisha.

Basi wadau tuishie hapo kwa leo...inshallah tukijaliwa tutaendelea kesho. Pia niwashukuru kwa maoni yenu hasa wale ambao hawakioni kisa hiki kama ni muhimu au msaada. Sina majibu ya kuwapa ila naamini wapo wanajamii wenzangu wanahamu ya kutaka kujua mwisho wake au walishakutana na kisa kinachofanana na hiki. 

Ahsanteni.

No comments