BWANA HARUSI ALIYEMKIMBIA MKEWE KANISANI MBEYA ARUDI NYUMBANI


Harusi, Samuel Mwakalobo aliyetoweka muda mfupi kabla ya kufunga ndoa na Given Mgaya katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Isanga jijini hapa, amerudi nyumbani kwao juzi.

Kaka wa bwana harusi huyo, Braison Mwandemele ambaye ndiye aliyemlea, alisema alirudi nyumbani akiwa salama, lakini amepumzishwa bila kuulizwa lolote.


“Sijaongea naye lolote, yupo kwenye mapumziko, hivyo tunaomba mtuache kwanza,’’ Mwandemele alisema jana.


Mwakalobo (26) alizua taharuki Ijumaa ya Desemba 16, baada ya kutoonekana kanisani kufunga ndoa mbele ya Mchungaji Andagile Mwakijungu.


Kuhusu tukio hilo, Mchungaji Mwakijungu alisema ni la aina yake na linahitaji maombezi wala siyo kuzungumzazungumza ovyo.


Alisema aliitangaza ndoa hiyo siku 21 kanisani hapo kwa mujibu wa sheria na hapakuwa na pingamizi lolote na kwamba Alhamisi jioni (siku moja kabla ya harusi) alikutana wanandoa watarajiwa wote wawili na kuzungumza nao huku kila mmoja akiwa ni mwenye furaha na wakipeana miadi ya kuwahi ili wamalize mapema shughuli ya kuwaunganisha kimwili.


Mchunganji huyo alisema baada ya kuona tukio hilo limechukua sura mpya, alimuuliza bibi harusi kama kuna shida yoyote iliyojitokeza na kujibiwa kwamba hapakuwa na jambo lolote na kwamba hata yeye alishangaa kutomuona bwana wake wakati ndiye aliyempa hata fedha ya kwenda saluni.

No comments