Utafiti: Kuangalia TV kupita kiasi hupunguza uwezo wa kuzalisha mbegu za kiume
Kuangalia TV ni sehemu ya maisha ya asilimia kubwa ya watu duniani hivi sasa, lakini utafiti umeonesha kuwa wanaume wako kwenye hatari ya kupungua uwezo wa kuzalisha mbegu za kiume pale wanapotumia muda mwingi kuangalia TV.
Kabla hujaanza kubisha, soma kwa makini utafiti huu. Wenzetu husema ‘no research no right to speak’.
Utafiti huo ulifanywa hivi karibuni na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Copenhagen, umeonesha matokeo hayo baada ya kutumia sampuli ya vijana wa kiume 1,200.
Utafiti huo uliochapishwa kwenye Jarida la Marekani la ‘Epidemiology’ ulionesha kuwa wanaume wanaopenda kuangalia TV (kwa saa tano na zaidi) walitoa wastani wa mbegu za kiume (sperm counts) milioni 37 kwa mililita moja, huku wale ambao hawakuwa na tabia ya kuangalia TV kabisa walitoa wastani wa mbegu za kiume milioni 52 kwa mililita moja.
Mwanaume huwa katika hali ya kawaida pale anapokuwa na wastani wa mbegu milioni 40 kwa mililita moja hadi milioni 300 kwa mililita moja. Lakini kuwa na kiwango cha mbegu chini ya milioni 10 kwa mililita moja huchukuliwa kama kiwango duni cha uzalishaji wa mbegu za kiume.
Katika sababu zilizotolewa kufikia matokeo hayo, wataalam hao wameeleza kuwa huenda hilo hutokana na ukweli kuwa wanaume wanaotumia zaidi ya saa 5 kuangalia TV hukosa muda mzuri wa kufanya mazoezi na kula kiafya, mambo ambayo ni muhimu kwa afya ya uzazi wa mwanaume
No comments