Madhara ya Unywaji Pombe kwa Mama Mjamzito
Mtoto
awapo tumboni hupata chakula (maji na virutubisho lishe) vyote kupitia
kwa mama yake. Mama akila mlo ulio kamili awapo mja mzito mtoto pia
hupata mlo kamili na iwapo mama hapati mlo kamili huwa hivyo kwa mtoto
pia. Je mtoto anakulaje awapo tumboni? Chakula huingia mwilini kwa mtoto
anayekuwa tumboni mwa mama yake kupitia kondo la nyuma au ‘placenta’
kwa Kiingereza. Hivyo mama anywapo pombe vilevile nayo huingia kwa mtoto
kupitia kondo la nyuma.
Pombe hujipenyeza kwa kasi katika kondo la nyuma la mama na kiwango cha
kilevi katika mwili wa mtoto (blood alcohol level) huwa sawa na kiwango
cha pombe kilichomo katika mwili wa mama. Kwamba humuoni mtoto awapo
tumboni si hoja sana kwani ushahidi unaonyesha kwamba athari za unywaji
pombe wa mama una matokeo hasi katika ukuaji wa mtoto. Yaani baadhi ya
athari huwa na matokeo ya kudumu ikiwa ni pamoja na kudumaa kwa akili za
mtoto pindi anapozaliwa, madhara ya jumla katika ukuaji wa mwili hasaa
ubongo wa mtoto.
Iwapo ulikunywa pombe ukiwa mjamzito, je ni zipi dalili za athari za
pombe kwa mtoto? Ingawa dalili ni nyingi, makala haya yatajikita katika
dalili za kudumaa kwa akili ya mtoto baada ya kuzaliwa. Mtoto mwenye
tatizo hili hupata taabu kuwakumbuka ndugu na jamaa wa karibu hata wale
anaoshinda nao nyumbani.
Ingawa watoto wa umri huu hupendelea kucheza na vitu vinavyowazunguka,
mtoto huyu hapendi ‘kujishughulisha’ na vitu vinavyomzunguka.
Unashauriwa kumpeleka mtoto kwa wataalamu wa afya kupata msaada zaidi
pindi unapohisi mtoto ana tatizo.
Mwongozo wa kitaalamu wa makuzi ya mtoto unaonesha kwamba mtoto wa umri
wa miezi sita anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya mengi ya mambo
yafuatayo; toka anazaliwa anapaswa kuweza kugeuza shingo lake kufuata
mwelekeo sauti inakotokea, aweze kushika miguu yake akiwa amelala
kifudifudi, aweze kukuangalia anapokuwa ananyonya / kula, aweze
kutabasamu aonapo nyuso na kusikia sauti za watu anaowafahamu, aweze
kulia anapoudhiwa / ama akiwa hajisikii vizuri (mgonjwa, njaa, nk.),
apate kutoa sauti mbalimbali ikiwapo kwikwi ndogondogo na hata kupiga
kelele na mwisho awe na tabia ya kutaka kutia kila akishikacho mdomoni
mwake.
Moja ya njia kuu za kumlinda mtoto na madhara yatokanayo na unywaji
pombe ni kwako mama mjamzito kuacha kunywa pombe mara tu unapogundua una
ujauzito. Iwapo huwezi kabisa kuacha kunywa pombe basi unashauriwa
kwenda kwa daktari na kupata ushauri zaidi. Kumbuka kuacha kunywa pombe
katika hatua yoyote ya ujauzito kutakuongezea nafasi ya kujifungua mtoto
mwenye afya na siha njema.
No comments