Ukweli kuhusu kupata watoto mapacha
Inasemekana kwamba haijalishi kama
mume/mwenza wako ni pacha ama ametoka kwenye familia yenye historia ya
mapacha. Mwenye uwezo wa kusababisha watoto mapacha ni mwanamke pekee.
Ikiwa na maana mwanamke ambaye ni pacha ama ndugu zake wa kike kama vile
dada, mama wana historia ya kuwa na mapacha ama wao ni pacha basi
mwanamke huyo ana nafasi kubwa ya kupata watoto mapacha.
kwa mfano: Mwanamke ambaye mke wa mjomba
wake ana mapacha haimpi yeye nafasi ya kupata mapacha kwa sababu hana
uhusiano na mke wa mjomba wake kibailojia. Ila mwanamke ambaye dada yake
ana mapacha inampa uwezekano wa kupata watoto mapacha kwasababu wana
uhusiano wa moja kwa moja.
Hembu tujifunze hatua moja baada ya
nyingine. Kwanza tufahamu mimba inatungwa vipi? Na kisha tuone jinsi
gani mimba ya watoto mapacha inavyotungwa.
Mimba inatungwaje?
Kipindi cha ovulation ndipo ambapo
mwanamke anaweza kushika mimba. Ovulation ni kipindi ambacho yai kubwa
ama yai lililo tayari hutoka kuelekea kwenye tumbo la uzazi kupitia
mirija ya ovari. Yai hilo kwa bahati nzuri likikutana na mbegu ya kiume
hurutubishwa katika kipindi cha masaa 24 (baada ya muda huo yai hupoteza
uwezo wake). Iwapo yai litarutubishwa ndani ya muda huo na kisha
kujikita katika mfuko wa uzazi basi mimba itakuwa imetungwa. Iwapo yai
halikurutubishwa hutolewa nje kama damu ya hedhi.
Mapacha hutokeaje?
Hapa tukumbuke kuwa kuna mapacha wa aina
mbili: Mapacha wanaofanana (Identical twins) na Mapacha wasiofanana
(Fraternal twins). Mapacha wasiofanana hutokea pale mwanamke anapotoa
mayai mawili kuelekea kwenye tumbo la uzazi. Hii ina maana ni mwanamke
ama mwili wa mwanamke unaosababisha mayai mawili kuachiliwa kwa pamoja.
Baada ya hapo mayai haya hukutana na mbegu za kiume ambapo hurutubishwa
ndani ya muda maalumu na kisha hujikita kwenye mfuko wa uzazi. Hivyo
basi hata kama mwanaume angetoa mbegu milioni moja lakini yai la
mwanamke likitoka moja basi mtoto atakayepatikana atakuwa ni mmoja tu.
Huo ni upande wa mapacha wasiofanana
(Fraternal twins). Kwa upande wa mapacha wanaofanana (Identical twins)
hadithi ni tofauti kidogo. Baada ya yai kurutubishwa na mbegu ya kiume
na kujikita kwenye mfuko wa uzazi kwa sababu zisizofahamika kisayansi
huamua kujigawa na kutengeneza watoto mapacha. Mapacha hawa kwa kawaida
hufanana sana na huwa ni wa jinsia moja tofauti na fraternal twins ambao
huweza kuwa wa jinsia mbili tofauti ama jinsia moja.
Kutokana na maelezo hayo hapo juu
inaonyesha kwamba watoto mapacha wanaofanana ama wasiofanana husababisha
na mwanamke ambaye kwa sababu moja ama nyingine mwili wake huachilia
mayai mawili ama hugawanya yai lake lililorutubishwa na kusababisha
watoto mapacha. Japokuwa kumekuwa na mabishano makali ambapo watu
wengine wamekuwa na maoni hususani kwa upande wa mapacha wanaofanana kwa
kusema kwamba mbegu ya kiume huwa na nguvu zaidi na hivyo kugawanya
yai. Sina uhakika na jambo hilo ila kwa tafiti nyingi zilizofanywa na
wanasayansi zinasema mwanamke ndiye mwenye uwezo wa kusababisha watoto
mapacha yeye ama ndugu zake wa kike (wanaohusiana kibaiolojia).
Sababu nyingine zinazoweza kuchangia watoto mapacha
1. Mwanamke anayetoka kwenye familia ambayo wanawake wana historia ya kupata mapacha.
2. Wanawake wenye asili ya kiafrika na kimarekani.
3. Wanawake wanaobeba mimba wakiwa na umri mkubwa, kuanzia miaka 35.
4. Wanawake wanene na wale warefu.
Hitimisho
Kwa kifupi kama huna sababu zilizotajwa
haina maana kwamba hauna uwezo wa kupata watoto mapacha. Uwezekano huo
upo ila ni kwa kiwango kidogo kama wanawake wengine duniani. Kumbuka
sababu zilizotajwa hapo juu hazihusiani na mapacha wanaofanana,
inavyosemekana mwanamke yoyote ana uwezo wa kupata mapacha wanaofanana
hata kama kwenye familia yake hakuna historia hiyo.
Tahadhari
Maelezo yote yaliyotolewa hapa hayana
maana kwamba ndiyo ukweli kwa asilimia mia moja la hasha kuna baadhi ya
watu kwenye familia zao wanaamini kwamba watoto mapacha waliowapata
wametokana na upande wa baba. Ila kwa asilimia kubwa inavyosemekana na
wataalam wa masuala ya uzazi watoto mapacha husababishwa na mama pamoja
na wanawake kutoka kwenye familia yake. Kama unataka kujifunza zaidi
nakushauri soma zaidi tafiti mbalimbali.
Ukweli kuhusu kupata watoto mapacha
Reviewed by Unknown
on
June 11, 2018
Rating: 5
No comments