Unataka kufanikiwa kimaisha??? hizi hapa mbinu
Kwanza, kabla sijaendelea embu tuwekane sawa kuhus hii falsafa ya
“kufanikiwa kimaisha”, ina maana gani haswa? Ukweli ni kwamba watu wengi
wakisikia fulani amefanikiwa kimaisha, basi moja kwa moja wanafikiri au
wanaamini mtu huyo atakuwa na pesa nyingiiii au kwa maneno mengine, mtu
huyo ni tajiri fulani hivi. Pamoja na kwamba pesa ndio mtatuzi wa
mahitaji mengi hapa duniani, lazima tukumbuke kwamba pesa ina uwezo wa
kununulia kitanda cha gharama kubwa sana, lakini ukashindwa kulala
katika kitanda hicho kwa msongo wa mawazo. Pia pesa inaweza ikakufanya
uopoe mwenza mzuri kuliko wote duniani, lakini mwenza huyo asiwe na
mapenzi ya dhati kwako.
Hapa tunajifunza kwamba ingawa pesa ni muhimu sana maishani, kufanikiwa
au kutofanikiwa kwa mtu kimaisha hakuwezi kupimwa kwa kiasi tu cha pesa
alichonacho. Mtu anaweza akawa na pesa, lakini akakosa raha kutokana na
ukosefu wa amani ya ndani na nje ya mwili. Hivyo basi, Kufanikiwa au
kutofanikiwa maishani kwa mtu, ni lazima pia kupimwe kwa mambo mengine
muhimu kama uchamungu, ukarimu, maadili, busara, uvumilivu, na ujasiri
(wa kufanya na kuishi na maamuzi magumu). Hivi “viambatanisho” 6 vya
pesa ndio vinarutubisha na kudumisha pesa, na zaidi humfanya mtu
afurahie (enjoy) pesa hizo. Kwa uzoefu wangu, mchanganyiko wa mambo haya
yote muhimu, ndio humfanya mtu “afanikiwe kimaisha” kwa maana pana ya
falsafa hiyo. Baada ya muhtahsari huu, tuendelee sasa na mada yetu,
ambayo leo inagusia mambo makuu matano ya watu waliofanikiwa kama
ifutavyo:
#1: Huishi Kwa Siku Za Baadae (Future), Na Sio Siku Zilizopita (Past). Bila
shaka umeshasikia ule usemi wa siku nyingi kwamba “yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo”. Watu waliofanikiwa kimaisha huwa na tabia ya
kutokatishwa tamaa na mambo ambayo yameshapita, na hayakwenda kama
walivyotarajia, kwani siku zote huwa wanakubali matokeo ya kutofanikiwa
kwao katika suala fulani na kujipanga upya kulikabili suala hilo. Siku
zote hujizuia kuruhusu matukio ya kushindwa kwao kufanikiwa katika
masuala fulani maishani, kushusha imani yao yakufanikiwa katika masuala
ya baadae (future).
#2: Hawalii Shida Na Wala Hawana Kinyongo. Hisia
zako za siku kwa kiasi kikubwa zinategemea na wapi ulipoelekeza mawazo
yako. Kwa mujibu wa mtaalam wa Saikolojia, Travis Bradberry, anaweka
wazi kwamba “kama umeelekeza mawazo yako kwenye shida ambazo
zinakukabili, basi unajijengea hisia hasi mwilini na kujiongezea
mastresi kibao, ambayo yana athiri na kuzuia uwezo wako wa kufanya mambo
ya kimaendeleo”. Hivyo basi, watu waliofanikiwa maishani huwa
wanaelekeza mawazo yao kwenye masuala chanya, ili kupiga vita mastresi
na kujiongezea uwezo wa kukomaa na mambo ya maendeleo. Pia, watu
waliofanikiwa maishani huwa hawaendekezi kinyongo, kwani wanaelewa kuwa
kuweka kinyongo katika masuala yaliyopita ni hatari sana kwa maendeleo.
Vinyongo kama ilivyo kubebea shida mbeleko, ni vitu ambavyo huzalisha
hisia hasi mwilini na kumfanya mtu kuwa na mastresi (au msongo wa
mawazo), ambayo yana mzuia kufanya mambo ya maendeleo.
#3: Hawatoi Kipaumbele Katika Ukamilifu. Hapa
ina maanisha kwamba, watu waliofanikiwa maishani huwa hawapotezi muda
katika kutafuta ukamilifu (perfection) katika mambo yao. Ni watu, ambao
wanafaham kwamba binaadam ni viumbe dhaifu na ukamilifu ni wa Mungu peke
yake. Hivyo basi, hii sifa inawasaidia sana linapokuja suala la
kuridhika na kile walichoweza kufanya baada ya kujitahidi kwa uwezo wao.
Hii inawafanya waendelee kujiamini, badala ya kujilaumu na kujihisi
wamefeli kama wale watu wanaolenga ukamilifu katika ufanyaji wa mambo
yao.
#4: Hawapotezi Muda Wao Na Watu Wenye Mawazo Hasi. Hii
sifa ni muhimu sana na kwa ufupi ni muendelezo wa sifa #2, kwani ili
mtu aendelee kubaki na mawazo chanya kwa mustakbali mzima wa maendeleo
yake, ni lazima apinge kukaa na watu wenye mawazo hasi au walalamikaji.
Kwa ung’eng’e wanasema “ don’t hangout with negative people!” Hapa
wanazungumziwa marafiki, ndugu, na jamaa, yaani kuwa makini sana kuhusu
watu unaokaa na kuzungumza nao kwa siku. Kama watu hawa wamejaa
malalamiko tu kuhusu maisha yao siku nzima, basi jua wanagonjwa hatari
sana na ni watu wa kukaa nao mbali, ili wasikuambukize gonjwa hilo
hatari kwa maendeleo yako. Siku zote watu waliofanikiwa maishani (au
wale walio mbioni kufanikiwa) huwa wanajihusisha na watu wenye mawazo
chanya na matumaini tele kuhusu mustakbali wa maisha yao.
#5: Hawaoni Hatari Kusema “Hapana!”
Hii pia ni sifa muhimu sana, kwani watu wengi wanaostrago maishani, ni
watu ambao wanataka kumridhisha kila mtu, kitu ambacho ni kigumu sana.
Mbali na kwamba sifa moja wapo ya mtu aliyefanikiwa maishani ni ukarimu,
watu hawa pia wana ujasiri wa kusema hapana katika mambo ambayo
hawataki au hawana muda wa kufanya. Ni watu ambao hawazunguki mbuyu
linapokuja suala la kumwambia mtu kwamba ombi lao kwao limekataliwa.
Hapa sio tu kwa wale watu wanaopenda kupiga mizinga ya pesa (ambayo
mengine haina msingi wowote), bali pia kusema hapana linapokuja suala la
kuombwa msaada wa kikazi na washirika wa biashara au ajira. Watu
waliofanikiwa maishani hawaoni hatari kukataa kutoa msaada wa kikazi kwa
watu wengine, ili kujipa muda zaidi na uwezo wa kufanya kazi zao.
Anza kufanya uchunguzi wako leo kwa watu unaowafaham, ambao
“wamefanikiwa maishani” na utaona mifano hai ya sifa hizi au kama tayari
unawafaham watu hao, basi tupe maoni yako kwa faida ya wasomaji wote!
No comments