UMEUMIZWA PENZINI? CHUKUA SIRI YA USHINDI!
MAPENZI yanauma. Yanauma kwelikweli. Unapokuwa umewekeza nguvu, mwili na
akili kwa mtu halafu ikatokea amekatisha safari ghafla huwa inauma.
Inauma sababu ulikuwa na maono ya mbali na penzi lako. Unaumia kwa
sababu hukutegemea kama safari ya uhusiano wenu itaishia katika hatua
hiyo. Inawezekana ulifikiri kwamba mngefika kwenye hatua ya ndoa lakini
haikuwa hivyo.
Yawezekana ulikuwa na ndoto ya kuwa na familia, uitwe baba au mama.
Ulikuwa unatamani kuzaa na mwanaume au mwanamke wa ndoto yako lakini
kumbe sio.
Anaondoka kwenye kipindi ambacho wewe bado unamhitaji.
Leo nataka nikupe siri ya ushindi kupitia safu hii. Inapotokea umeumizwa
penzini, unachotakiwa kufanya ni kutulia. Itulize akili yako vizuri na
usiiweke kwenye mawazo hata kidogo. Muhimu ni kukubaliana na kitendo
kilichotokea.
Kama mwanaume au mwanamke wako amekuacha, kubali. Ona kwamba kuna sababu
za wewe kukuacha lakini usihangaike nazo sana wakati huo maana
zitakutesa bure tu.
Kuanza kuwaza kwamba labda sijui amekuacha sababu wewe si mzuri, kwamba huna fedha, utaumia tu!
Kuwaza kwamba sijui una upungufu gani, sijui kwa nini ni wewe kila siku unaumizwa ni makosa makubwa.
Kubaliana na matokeo haraka. Ifanye
akili yako iwaze vitu vipya hata kama uliyekuwa naye ulimpenda kiasi gani.
Ameshaamua kukuacha, ana sababu zake hivyo ukiendelea kupigana kuzijua
hizo sababu ni kazi bure. Muache aende na wewe utakuwa kwenye nafasi
nzuri ya kuingia kwenye uhusiano mwingine hapo baadaye kama aliyekuacha
hatajirudi.
Marafiki zangu, maisha ya uhusiano yana siri kubwa sana. Kila mmoja
kwenye historia ya uhusiano na mwenzi wake anapitia mengi hadi kufikia
hatua ya kuingia kwenye ndoa. Wakati mwingine inakuwa hata ni vigumu
kujua kwamba atakayekuoa au kumuoa ni nani.
Unaingia na mtu kwenye uhusiano, mnaishi miaka miwili mitatu mnaachana. Unaingia kwenye uhusiano na mtu mwingine, mnaachana.
Unarudi kwa yule wa awali, mnakaa kipindi fulani lakini wapi. Kidudu mtu anaingia, uhusiano unayumba tena.
Unavurugwa mno. Unajiona kama huna bahati na unasahau kwamba maisha ya
uhusiano ndivyo yalivyo. Unayekwenda kuingia naye kwenye ndoa wakati
mwingine ni vigumu sana kumjua. Akili za kibinadamu mara nyingi
zinatudanganya tu.
Ndugu zangu, licha ya kwamba sisi binadamu tuna macho yetu na akili
lakini juu ya nani hasa unakwenda kuingia naye kwenye ndoa huwa ni Mungu
ndiye ajuaye.
Mungu anatujua sisi tangu tukiwa matumboni mwa mama zetu. Anajua mahitaji ya maisha yetu kabla hata hatujamuomba.
Tunahangaika na dunia yetu hii ya uzuri wa sura. Tunapagawa na mambo ya kidunia lakini unganiko la ndoa alijuaye ni yeye pekee.
Unapoona kuna janga limetokea kwenye uhusiano wako, mshukuru Mungu tamka neno hili; ‘hili nalo litapita.’
Kama aliyekuacha amepangwa awe wako atakuwa. Kama hajapangwa basi
atakuja ambaye ni sahihi. Cha msingi wewe sema tu na moyo wako. Tamka
tena maneno haya; ‘ipo siku tu.’ Maneno hayo matatu ni muhimu katika
mustakabali wa furaha yako.
Yatakufariji. Yatakutia nguvu ya kuendelea na maisha upya hata kama umeumia kiasi gani, utasema lazima maisha yaendelee.
Kataa kuwa mtu wa mateso kila siku. Usiwaze sababu kama huyo ameondoka na si wako basi amini kwamba ipo siku atakuja mtu sahihi.
Utashanga atakapokuja mambo yananyooka tu yenyewe bila hata kutumia
nguvu nyingi. Mwezi wa kwanza wa pili mambo yanajipa. Mnaingia kwenye
ndoa na maisha yanakuwa ni bambam.
No comments