Jinsi Mwanamke Anavyoweza Kuongeza Hips na Makalio kwa Mazoezi ya Viungo



Baadhi ya wasichana huwa hawaridhiki na maumbile yao ya asili, wengine hupenda kuwa wembamba hasa pale mtindo wa maisha au maumbile yao ya asili yanapowalazimisha kunenepa. Na wengine hupenda kunenepa au kunenepesha baadhi ya sehemu za miili yao kama vile makalio, mapaja (hips) au matiti. Wengine hupenda kuona matiti yao yakiendelea kusimama miaka yote ya maisha yao na kuwa kama ya wasichana wanaoanza kubalehe.

Kutokana na sababu hizi na sababu za kuongeza mvuto wao kwa wanaume au kujitangaza kibiashara, wasichana na wanawake wengine hulazimika kutumia njia mbadala za kunenepesha sehemu za miili yao. Wengi hutumia mavazi maalumu kwa kazi hiyo (pads and shape wear), dawa za kupaka au sindano za kunenepesha makalio, mapaja na kutunisha matiti na wengine hutumia njia za asili kama vile mazoezi ya mwili au dawa za mitishamba au dawa zijulikanazo kwa jina maarufu la ‘dawa za kichina’
Kimsingi unenepeshaji wa kisasa wa makalio, mapaja na matiti hufanyika kwa njia ya kuweka vipandikizi (silicone implants), kupaka cream, kuchoma sindano za mafuta ya mwili kutoka katika nyama za tumbo (fat transfer injection) au kuvaa vitu vinavyotengeneza umbo linalotamaniwa na wanaume. Mambo haya hufanyika katika kliniki maalumu na yanaweza kugharimu pesa nyingi.

Matumizi ya dawa za kunenepesha makalio, mapaja na kutunisha matiti si salama kwa afya kwani zinaweza kusababisha hali ya kushindwa kupumua kutokana na mzio (allergy), kansa, kuoza kwa misuli ya makalio na miguu (gangrene), uvimbe wa misuli (lumps/granuloma), kunenepa kwa makalio au matiti bila mpangilio au ulinganifu, kupooza au kifo wakati mwingine.

Dawa hizi zinaweza kusababisha kifo pale zinapoingia katika mfumo wa damu na kaharibu ini, ubongo, moyo na mapafu. Dawa zingine kutokana na kuongezewa viambato vya steroidi, mapema au baadaye sana zinaweza kusababisha magonjwa ya vidonda vya tumbo, udhaifu wa mifupa (osteoporosis), figo kushindwa kufanya kazi na shinikizo la damu.
Hata dawa za asili zitokanazo na mitishamba kama vile Mvunge au Miegeya (Kigelia Africana) ambazo hutumika sana kwa ajili ya kazi hii, bado uwezo wake na athari zake havijafanyiwa utafiti wa kutosha kisayansi ili kubaini usalama wake hasa kuhusiana na hatari ya kansa ya ngozi.

Kuna mifano mingi ya wanawake waliodhurika au kupoteza maisha kutokana na dawa hizi za urembo usiokuwa wa lazima. Mwaka 2004, mwanadada Apryl Michelle Brown mwanamitindo ya urembo wa nywele (Hair stylist) kutoka Los Angeles, Marekani alipoteza makalio, mikono na miguu yote baada ya misuli yake kuoza kutokana na kupata madhara ya sindano za kunenepesha makalio. Mrembo wa zamani wa Argentina(1994), Miss Solange Maginano akiwa na umri wa 38, alifariki dunia mnamo mwaka 2009 katika Kliniki moja huko Buenos Aires, Argentina akiwa anapewa dawa za kuongeza ukubwa wa makalio yake.

Mwaka 2011, kulikuwa na taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa Claudia Adelotimi, mwanadada mwenye asili ya Nigeria aliyekuwa na umri wa miaka 20 akifikiri kuwa kunenepesha makalio kungemfanye awe nyota katika ushiriki wake kwenye picha za video za muziki wa kizazi kipya wa kufokafoka, alipoteza maisha kwa kuchoma sindano hizi huko Philadephia, Marekani baada ya kusafiri toka London, Uingereza na kulipia kiasi cha fedha kinachokadiliwa kuwa £ 1,300.

Visa vya namna hii ni vingi sana miongoni mwa wasichana na wanawake wanaopenda urembo bila kujali afya kwanza. Wasichana wengi wanapotumia dawa hizi, huwa wanafikiri kuwa wanaboresha muonekano na maisha yao lakini wanapopata madhara ya kiafya, hupoteza vyote yaani ubora wa maisha na uzuri wao wa asili na kubakia na majuto ya kudumu.

Kwa wasichana ambao wanaona kuwa maisha hayawezi kuwa matamu bila kunenepesha makalio, mapaja na matiti yao, ni busara kufanya hivyo kwa njia za asili zisizokuwa na madhara kwa afya zao. Sehemu hizi za mwili zinaweza kunenepeshwa kwa kutumia sayansi ya lishe bora, kunywa maji mengi na mazoezi ya mwili.
Kula vyakula vyenye protini ya kutosha na vyakula vyenye asili ya mimea yaani mbogamboga, matunda, nafaka zisizokobolewa na mafuta yenye asili ya mimea pamoja na kupunguza sukari na chumvi kwenye chakula, husaidia sana katika uimarishaji na unenepeshaji wa misuli ya makalio, matiti na mapaja. Kuepuka ulaji wa nyama yenye mafuta mengi au mazao ya maziwa kama vile siagi na samli pia husaidia.

Mazoezi ya kila siku (asubuhi na jioni) ya kupunguza mafuta katika nyama za tumbo, kufanya kiuno kuwa chembamba na kuimarisha misuli ya mapaja pamoja na makalio ni njia bora ya kumpatia msichana umbo la kupendeza na kunenepesha au kutunisha makalio bila madhara ya kiafya.
Baadhi ya watafiti na wataalamu wa mambo ya urembo wanadai kuwa, kiuno cha msichana au mwanamke chenye uwiano wa 70% ya mzunguko wa mapaja yake (hips circumference) au kipimo cha 0.7 WHR (waist to hip ratio) kinaonyesha afya nzuri ya msichana au mwanamke na kinafanya makalio na mapaja ya msichana au mwanake kuonekana kuwa makubwa.

Mazoezi yanayosaidia katika jitihada za kufikia lengo hili kwa kutumia njia za asili na kwa usalama huku yakiimarisha afya ni pamoja na kuruka juu, kupanda ngazi za nyumba (stair climbing), kuinama, kuchuchumaa pamoja na kuminya au kuchua misuli ya makalio (massage) kila siku.

Ili zoezi la kuchuchumaa lilete matokeo yanayokusudiwa fuata kanuni zifuatazo: Kwanza tambua kuwa lengo lako ni kubadilisha muonekano wa umbo lako kwa njia salama, hivyo basi ni lazima ujitume kufikia lengo hilo. Anza mazoezi ya kusimama wakati miguu yako ikiwa imeachana kiasi cha upana wa kifua chako kisha taratibu kunja miguu yako kwenye magoti ili kuchuchumaa hadi mapaja yawe sambamba na sakafu au ardhi kwa dakika kadhaa kisha panda juu taratibu ili usimame kama mwanzo. Fanya zoezi hili angalau mara ishirini kabla hujapumzika au kubadilisha mtindo wa zoezi.

Fanya mtindo mwingine wa zoezi la kuchuchumaa wakati miguu ikiwa imepishana, weka mguu mmoja mbele kiasi cha umbali wa hatua moja na mguu mwingine uwe nyuma kisha chuchumaa kwa kukunja magoti yote, mguu wa mbele ujikunje na kutengeneza kona yenye 90° digrii na mguu wa nyuma uwe chini kiasi cha nchi 2 hivi juu ya sakafu. Kisha simama na kubadilisha mguu uliokuwa nyuma uwe mbele na kurudiarudia zoezi mara kwa mara.
Zoezi jingine ni lile la kuweka magoti yote na viganja vya mikono yote sakafuni kama mtu anayetaka kusujudu, kisha inua mguu mmoja kwa nyuma wakati goti moja na mikono ikiwa sakafuni. Badilishabadilisha mguu wa kuinua na fanya hivyo kwa dakika 20 kila siku asubuhi na jioni. Lakini pia unaweza kusimama wima na kunyoosha mikono yako yote mbele usawa wa kifua chako kisha ishushe taratibu hadi uguse vidole vya miguu yako kwa mikono yote miwili. Baada ya hapo inuka taratibu hadi usimame wima kama mwanzo na urudierudie zoezi hili kwa dakika 20.

Zoezi jingine linaloweza kusaidia ni lile la kuchua au kiminyaminya misuli ya makalio (massage) kwa dakika 30, asubuhi na jioni kila siku. Zoezi hili huimarisha misuli na kuongeza kiasi cha mzunguko wa damu katika nyama za makalio. Zoezi la kuchua misuli pia linaweza kusaidia katika utunishaji wa matiti kwa wale wanaohitaji matiti makubwa yaliyojaa.

Fanya massage ya matiti kwa kutumia vikanja vyako kila siku asubuhi na jioni na kuchezea chezea chuchu kwa dakika 30, hii itaongeza mzunguko wa damu katika matiti na kupunguza damu ya hedhi lakini pia itasababisha ongezeko la kichocheo cha prolactin na kuimarisha misuli ya matiti. Ili mazoezi haya yalete matokeo yaliyokusudiwa ni lazima yawe endelevu na yaende sambamba na kanuni zingine za afya na urembo kama vile lishe bora, kunywa maji ya kutosha na kuwa na mtazamo chanya katika maisha.

No comments