kama unataka kudumisha uhusiano wako udumu kwa muda mrefu. Zingatia mambo yafuatayo




Jambo la 1.
Endelea kufanya vitu ulivyokuwa unafanya wakati uhusiano wenu unaanza- Mara nyingi tumekuwa tukijisahau katika mahusiano. Tukishakaa muda tukazoeana tunaona inatosha na tunasahau kufanya vile vitu tulivyokuwa tunavifanya awali ambavyo pengine ndivyo vilivyomvutia mpenzi wako mpaka akaamua kuwa na wewe. Kwa mfano wakati mnaanza mahusiano mlikuwa mnatumiana ujumbe, siku haipiti bila kuwasiliana, mnaitana majina mazuri ya kimapenzi kama vile ‘darling’, ‘baby’, ‘sweetheart’ na mengineyo ya namna hiyo. Lakini mkishazoeana basi majina hayo hutoweka, mtu anashinda siku nzima hata kumjulia hali mpenzi wake hakuna tena. Sasa ikishafikia hatua hii ndiyo tunaacha mwaya wa michepuko wewe si hautumi meseji bwana, basi wapo wenzio wanaojua kutuma meseji tena kila baada ya dakika moja meseji inaingia. Kama wewe haumwiti tena ‘baby’ basi fahamu kuna wengine wanafanya hivyo. Kila mtu  anapenda kupendwa, kujaliwa na kuthaminiwa na hapa hakuna cha mwanaume wala mwanamke wote sawa. Jitahidi sana kufanya yale yote uliyokuwa unafanya wakati uhusiano wenu unaanza hata kama si kwa asilimia mia moja lakini hakikisha haujisahau kabisa huwezi kujua mwenzio alikupendea nini.
Jambo la 2.
Zungumza unachohitaji- Mara nyingi tumekuwa tukiamini kwakuwa umeishi na mtu kwa miaka mingi ama upo kwenye uhusiano kwa muda mrefu basi tayari mpenzio anajua uchohitaji hata bila kumwambia na kasheshe ni pale ambapo unaamini anajua halafu hatimizi. Sasa ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima tujifunze kunzungumza. Mpenzi wako siyo malaika ama mtabiri aweze tu kujua unachokihitaji. Wakati mwingine labda ni sikukuu ama weekend unatamani kutoka out lakini husemi unaamini mpenzio atajua unataka kwenda out. Seriously? hembu acha utani zungumza. Katika yale mambo yetu ya chumbani sasa, tena hii ni kwa wanawake zaidi, unakuta unahitaji huduma  lakini usemi. Wengine hujitahidi kuonyesha vi ishara ishara na vimitegotego  sasa ndiyo visipoeleweka utajua balaa lake, mtu atakasirika na kuzira kimoyomoyo na kuona hapendwi, Zungumza bwana mwenzio atajuaje kama unataka? Dawa ni moja tu kuzungumza unachokitaka ukiona mwenzako hakuelewi pamoja na ishara zako kibao wewe mwambie tu.  Tuachane na tabia za kutaka kuonekana babkubwa kumbe unaumia moyoni. Shauri zako usipozungumza, wenzio watakusaidia kuzungumza.
Jambo la 3.
Mjue mpenzi wako vizuri- Hakikisha unamjua vilivyo mpenzi wako. Anza kwa kufahamu vitu anavyopenda na vitu anavyochukia halafu jitahidi sana kutokufanya asivyovipenda hasa mbele yake. Fahamu akiwa amechoka anakuwaje, akiwa hana raha anakuwaje, akiwa na furaha anakuwa, hii itakusaidia kumfariji, kumtia moyo kutokana na hali anayokuwa nayo. Siyo mwenzio yupo kwenye huzuri wewe unamjia na habari zingine sijui kuna harusi ya nani na nani. Jifunze kusoma alama za nyakati siyo unakurupuka na ndiyo maana mwishowe wengine wanaishia kupewa majibu ya kutia kichefuchefu mpaka wanatamani kulamba ndimu. Vile vile kwa wale walio kwenye ndoa hakikisha unaujua vizuri mwili wa mpenzio kuliko hata vile unavyoujua mwili wako. Jifunze sehemu zote ambazo ukimgusa anafurahi na kusisimka. Halafu najua tu wengine wataenda moja kwa moja kwa wake/waume zao na kuwauliza eti sehemu gani nikikushika unafurahi. Ebo! hivi vingine hupaswi kuuliza unatakiwa uvijue mwenyewe na ukiona mwenzio anafikia hatua ya kukuambia mwenyewe jua hujafanya homework yako vizuri na pengine ni wakati wa kurudi jandoni na unyagoni. Illa kwa kifupi ninachomaanisha hakikisha unamjua mpenzio vizuri kwasababu itakusaidia kuishi naye katika hali yoyote atakayokuwa nayo.
Jambo la 4.
Jifunze kuomba msamaha. Umekosea na unajua umekosea hakuna namna yoyote yakumfanya mpenzi wako afurahi zaidi ya kuomba msamaha. Najua hili ni jambo gumu sana kwa wanaume lakini hamna ujanja ukikosa lazima uombe msamaha. La sivyo utadhani mwenzio kasahau kumbe amehifadhi moyoni. Kwanini? kwasababu ulishindwa kuomba msamaha. Kama vipi fumba tu macho omba msamaha, kwani ukifumba macho kuna mtu anakuona? Ili ukweli utabaki palepale mtu akikukosea halafu akakuomba msamaha hujisikia vizuri na ndiyo hivyo mpenzio atakavyofarijika pale utakapotambua kosa na kuomba msamaha. Unaweza hata ukaleta viji zawadi vya hapa na pale kuonyesha ni kwa jinsi gani umejutia ulichokifanya. Huu si utumwa jamani ndiyo mahaba.

No comments