Unawezaje kuwa na Uhusiano mzuri na watu usiofahamiana nao sana?




Mara nyingi imekuwa ni vigumu sana kuanzisha uhusiano/kuwa na uhusiano mzuri na watu usiofahamiana nao vizuri. Hembu fikiria hali unayokuwa nayo pale unapohamia kwenye mtaa mpya, ama kujiunga na chuo au pengine unapopata ajira mpya? Kila unayekutana naye ni mgeni, humjui hakujui unafanyaje kuhakikisha  unatengeneza mahusiano mazuri na watu hao?
Jambo la 1
Anza kwa kutoa salamu- Salamu  husaidia sana kujenga mahusiano mazuri na watu usiowafahamu. Watu wengi huchukizwa pale mtu anapopita bila kuwasalimu na hii huweza hata  kuanzisha uhasama mara moja. Jitahidi sana kutoa salamu inayoendana na watu wenyewe kama ni watu wazima wape salamu wanayostahili kama ni vijana wape salamu wanayostahili. Sasa usije ukachanganya madesa watu wazima unawaambia “Mambo zenu?” na kama si rahisi kujua rika la watu ni bora tu kusema ‘Habari za saa hizi?’ Maana siku hizi kuna watu wana miili mikubwa bwana unaweza ukadhani ni mtu mzima unamsalimia ‘Shikamoo mama” tena kwa adabu zote kumbe ni binti mbichi. Hii ni sababu tosha tu kwa yule uliyemkadiria umri vibaya kukuchukia. Cha msingi kuwa makini, toa salamu kwa nidhamu. Hembu fikiria unampita mtu bila kumsalimia halafu kumbe yeye ndiye anaweza kukupa msaada unaouhitaji, jasho litakutokaje sasa? Chukua tahadhari salamu haigombwi.
Jambo la 2.
Tabasamu- Wakati unatoa salamu pia jifunze kuweka tabasamu kwenye uso wako. Na unapokutana na watu katika kona mbalimbali jitahidi kutabasamu, mara nyingi unapompa mtu tabasamu na yeye hurudisha tabasamu. Hembu jaribu hili zoezi ukikutana na mtu hata kama haumjui wewe mpe bonge la tabasamu halafu uone kama na yeye hajatabasamu. Tabasamu huwafanya watu wajisikie huru kuzungumza na wewe. Ukiwa ndiyo mtu wa kuvaa sura ya kazi kama umelamba ndimu utashangaa watu wote wanakaa mbali na wewe. Utabaki kusema watu hawakupendi kumbe chanzo ni wewe mwenyewe. Kunjua ndita jifunze kutabasamu hasa unapopishana na watu uaotaka kujenga mahusiano nao.
Jambo 3.
Toa sifa- Kama mtu amefanya jambo zuri mpe sifa yake hata kama hamfahamiani sana. Hii pia ni njia nzuri ya kujenga mahusiano chanya. Kwa mfano mfanyakazi mwenzio amefanya kitu kizuri msifie, au amevaa gauni zuri limempendeza msifie. Acha wivu, tengeneza urafiki. Kanunua saa mpya onyesha umegundua na mpe maneno mazuri. Amini nakuambia kila mtu anapenda kusifiwa hata yule bosi wako unayemuona mkali kama mkoloni mjerumani naye pia anapenda kusifiwa.
Jambo 4.
Kuwa Mkarimu- Toa msaada pale inapowezekana kadiri ya uwezo wako. Labda mfanyakazi mwezio amelazwa na anahitaji damu na wewe unauwezo wa kuchangia jitolee. Hii pia ni njia nzuri ya kuwa na mahusiano mazuri na watu ambao walikuwa si marafiki zetu sana. Kwa mfano amekuja mfanyakazi mpya, jaribu kumwelekeza utaratibu hata kabla hajakuuliza. Jitambulishe na ikiwezekana mwambia akihitaji chochote upo kwa ajili yake hii itamfanya awe huru na kujenga uhusiano chanya na wewe.
Jambo 5.
Jifunze kusikiliza- Kila mtu anapenda kusikilizwa.  Upo mahali na kuna mtu anazungumza jambo fulani, sikiliza kwanza hata kama anaongea uongo sikiliza tu. Siyo kila muda unatakiwa kufungua mdomo na kurekebisha, wakati mwingine unachotakiwa kufanya ni kusikiliza labda kama una uhakika jambo analozungumza linaweza kuleta madhara hapo unaweza kuingilia kati lakini kama ni jambo tu la kawaida. Sikiliza tu ukishawazoea utazungumza na wewe. Mara nyingi watu hujisikia vibaya wakikosolewa na watu wasiowajua kuliko wale wanaowajua.
Hayo ni baadhi tu ya mambo kati ya mengi ambayo unaweza kuyafanya ili kudumisha uhusiano chanya hasa na watu ambao huwafamu vizuri na kuwanya wajisikie vizuri na huru unapokuwa karibu nao. Usiwe mtu ambaye ukiingia sehemu watu wote wananyamaza kimya mpaka utoke. Jitahidi uwe mtu unayeleta furaha na amani kila unapokwenda na vilevile si lazima watu wakupende unaweza ukafanya yote hayo hapo juu lakini bado watu wasikupende na kukubali. Lakini pamoja na hayo hauna sababu ya kuwachukia badala yake jifunze zaidi kuhusu wao ili uweze kwenda sawa na yale wanayoyapenda.

No comments