KAMA HUNA BAHATI YA KUPENDWA, TATIZO LIKO WAPI?

Mpenzi msomaji wangu, wiki iliyopita nilipata barua pepe kutoka kwa mmoja wa wasomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina moja la Joanitha.
Aliniandikia ujumbe mrefu sana juu ya kile kinachomsumbua kwenye maisha yake ya kimapenzi na akaniomba nimsaidie ili aweze kuwa na amani.Ujumbe wake huo ndiyo ulionisukuma kuandika makala haya kuelekea kwenye ile siku muhimu sana kwa wapendanao ya Valentine’s Day.
Aliandika hivi: “Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 25. Nimekaa kwa muda mrefu bila kuwa na mpenzi. Si kwamba napenda lakini nina kila sababu ya kusema, sina bahati ya kupendwa.
“Niliwahi kumpenda kaka mmoja ambaye alikuwa akiutesa moyo wangu kwa muda mrefu. Nilishindwa kujizuia na siku moja nilipokutana naye nilimueleza bayana kilichokuwa kikiusumbua moyo wangu. 
“Huwezi kuamini aliniambia wazi kuwa mimi siyo taipu yake, niliumia sana baada ya kugundua kuwa nilimpenda lakini hakuwa na mapenzi na mimi.
“Sikuishia hapo, nikatokea kumpenda kijana mwingine, naye alinipotezea. Sielewi nina kasoro gani. Mwenyewe nikijiangalia najiona ni msichana ninayestahili kuwa na mpenzi lakini simpati wa kunipa faraja. Naomba unisaidie anko.”
Ujumbe huo uliniumiza sana. Nikajua wapo wasichana wengi huko mtaani wanaohitaji wapenzi lakini hawawapati. Pia kuna wanaume wanaotokea kuwazimikia wasichana f’lani lakini kila wakijaribu kueleza hisia zao wanajikuta wanatolewa nje.
Kimsingi hali hiyo imekuwa ikiwatesa wengi lakini sasa swali la kujiuliza, ni kwa nini inatokea hivi? Inakuwaje mimi natokea kumpenda msichana f’lani lakini yeye hana taimu na mimi? Wanaojiuliza swali hilo ni wengi na kupata jibu kwa haraka ni ngumu hasa kama huna elimu ya kutosha kuhusu mapenzi.
Iko hivi, mapenzi yana kitu f’lani cha ajabu. Unaweza kushangaa inatokea mtu f’lani anakupenda sana lakini wewe huna taimu naye ila yupo ambaye na wewe unampenda lakini wala hakujali. Wataalam wa mapenzi wanaeleza kuwa, ni wachache sana waliopata bahati ya kuwapata watu wanaowapenda na ndiyo maana wengi wamebaki wakiumia kwa kutopendwa na watu waliotokea kuwapenda.
Watu kama hawa ndiyo wale ambao unawasikia wanaolewa na watu ambao hawawapendi, wanakubali tu kwa kuwa hawana jinsi. Matokeo yake sasa akiwa ndani ya ndoa kisha yule ambaye anampenda akajitokeza, ni rahisi sana kusaliti.
Hata hivyo, wale wasio na bahati ya kupendwa kama ilivyo kwa Joanitha wanatakiwa kujua kwamba, mapenzi yanahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Unaweza kukaa muda mrefu bila kuwa na mpenzi lakini huwezi kujua Mungu ana sababu gani.
Huenda hao ambao wewe unawapenda lakini wao wanakupotezea, siyo wale walipangiwa kuwa na wewe na endapo utalazimisha utakuja kujuta baadaye.Hatukatazwi kueleza hisia zetu kwa wale tuwapendao lakini tutarajie pia majibu hasi. Ujue kwamba huna haki ya kupendwa na kila utakayetokea kumpenda hivyo ikitokea umekosa uliyempenda, huna sababu ya kuumia.
Chukulia ni jambo la kawaida na huenda hiyo ndiyo safari ya kuelekea kumpata mtu atakayekupenda kwa dhati.Tuepuke kulazimisha kupendwa. Ukiona dalili kwamba unampenda lakini yeye hana chembe ya mapenzi kwako, kuwa mpole na muache. Nasema hivi kwa kuwa, wapo ambao wakitokea kupenda watafanya wawezavyo wafurahishe nafasi zao.

Hiyo ni hatari na nakuhakikishia kwamba, huwezi kupata penzi la kweli na badala yake utakuwa ni mtu wa kutendwa kila siku. Utasalitiwa, utaudhiwa na kamwe hutapata kile ulichokitarajia. Kwa nini? Kwa sababu uliyelazimisha awe na wewe, hakupendi kabisa.

No comments