Sababu Kuu 10 za Ugomvi kati ya Mke na Mme Katika Mahusiano
Ugomvi baina ya wapenzi katika mahusiano ni kitu cha kawaida kutokana na watu hao wawili kutoka katika malezi na mazingira tofauti ya ukuaji toka wakiwa wadogo hadi watu wazima.
Wawili hao wanapoaanza kujenga mahusiano na kukaa pamoja kama familia,kuna vitu kadhaa ambavyo kila mmoja wao huvitazama tofauti na hivyo kuleta migongano. Migongano ambayo inaweza ikarekebishika kama wenza hao watamua kuifanyia kazi na kuelewana.
Kuna vitu vingi ambavyo husababisha ugomvi na migongano ndani ya mahusiano ya mke na mme na hapa tunaeleza sababu kuu ambazo kwa kawaida hutokea karibu katika kila mahususiano
1. Wivu na Kukosa Kujiamini
Wivu unatokana na jinsi ambavyo mpenzi mmoja anavyohusiana na watu wengine wa jinsia tofauti. Inaweza ikawa marafiki,wafanyakazi wenza au wapenzi wa zamani. Vyovyote vile itakavyokuwa ni kwamba wivu unasababisha ugomvi katika mahusiano mengi.
Kunatakiwa kuweka mipaka ya kutosha na iliyo wazi ili kujenga uaminifu kwa mpenzi wako na kumpa kujiamini. Mpenzi ambaye hajiamini ni tatizo kubwa kwani uwezekano wa kuanzisha ugomvi ni mkubwa.Hivyo ni vizuri ukamjengea mweza wako katika mapenzi kujiamini kwa kuwa mwaminifu.
Uaminifu ni kitu kimoja kikubwa sana katika mapenzi. Kama mwenza wako akikuamini hakutakuwa na wivu wa kupita kiasi na pia atakuwa anajiamini kuwa yeye peke yake ndio chaguo lako na hakuna mwingine.
2. Mawasiliano Finyu
Mawasiliano yanapovunjika katika mahusiano ugomvi ni kitu cha kawaida kutokea.
Mawasiliano ya kawaida kati ya wapenzi husaidia sana kutoa wasiwasi wa nyendo za mwenza wako. Huleta amani na kujenga uaminifu kwa mpenzi kwako.
Kuzungumza juu ya mipango yako ya mendeleo kama ujenzi au biashara ni vitu ambavyo ni muhimu sana kuvifanya vinginevyo utajenga wasiwasi kwa mweza wako na itasababisha ugomvi wa mara kwa mara.
Kuwa muwazi kwa mipango ya maendeleo binafsi,ya familia yako na ndugu.
Utafiti unaonyesha kuwa wapenzi wanaoongea na kusikilizana mara kwa mara hawagombani mara nyingi kama wale wasio na mawasiliano ya kutosha.
3. Masuala ya Fedha
Japokuwa fedha si msingi wa mapenzi,lakini ni kitu ambacho kinahitajika sana katika maisha ya kila siku ya kila mtu na ya familia. Na kimekuwa ni mojawapo ya vitu ambavyo wapenzi katika mahusiano au ndoa hugombana sana juu yake.
Mwenza mmoja anapokuwa mtumiaji mbaya wa fedha na mwingine siyo,huibua malalamiko na ugomvi. Baadhi ya wapenzi hasa wanawake hawataki kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mahitaji ya msingi ya nyumbani na badala yake kuwaachia mzigo mkubwa wanaume.
Hili linaibua malalamiko mengi kwa baadhi ya wanaume,na wakati ungine toka kwa wanawake. Matumizi makubwa ya fedha kwaajili ya pombe na sharehe nyingine kwa wanaume na baadhi ya wanawake kumekuwa mojawapo ya sababu za ugomvi juu ya fedha katika mahusiano.
Ni muhimu kwa wenza wawili kupanga jinsi ambavyo fedha zao zitapatikana na kutumika. Vipaumbele vya kufanyika kwanza na kiasi cha kutumika kwajili ya starehe na urembo kwa wanawake kwa mfano.
4. Masuala ya Familia
Familia ya nani ianze kwanza na ipi ifuate ni tatizo kubwa katika mahusiano. Upendeleo wa upande mmoja ambao kwa asili huwa unatokea tu ni chanzo cha ugomvi ndani ya nyumba.
Mitazamo tofauti kati ya mmojawapo katika wapenzi na familia ya mwenza wake husababisha kutoelewana kwa wapenzi hao ndani ya nyumba.
Mbaya sana inakuja pale wanandugu wanapoingilia mambo ya ndani ya nyumba yenu. Wazazi wa kike na mawifi mfano, wamejulikana kusababisha matatizo mengi kwenye familia za watoto na kaka zao.
Kuepukana na hili ni muhimu kwa wapenzi ndani ya nyumba kuweka mipaka kwa ndugu ambayo haitaathiri uhusiano nao kama ndugu.
Pia ni muhimu kwa wenza hao kuweka mikakati ya pamoja juu ya kuhusiana nakusaidia ndugu toka katika familia zao mbili.
5. Suala la Unyumba
Japo kuwa suala kufanya mapenzi si kila kitu kwa wapenzi ndani ya nyumba lakini linachangia sana katika kuleta ugomvi aina yao. Kufanya mapenzi kupita kiasi au mara chache kunaleta matatizo kwa wapenzi hasa ambao wana uhitaji tofauti.
Wengine wanaona kama mpenzi ambaye hahitaji kufanya mapenzi mara nyingi na mwenzake labda anauhusiano na mtu mwingine zaidi yake. Au hamvutii tena kama zamani na huenda akaanza kuangalia nje.
Hii inajenga kutojiamini na kupoteza uaminifu,ambalo ni tatizo jingine kubwa katika mahusiano kama tulivyoonesha mwanzoni.
6. Vipaumbele katika Maisha
Wapenzi wawili wanapokuwa na mipango na malengo tofauti ni tatizo kubwa. Watu wanapokuwa katika uhusiano ambao ni wa kuishi daima,malengo na vipaumbele vyao ni lazima vioanishwe na juhudi za kila mmoja zilenge katika kufanikisha mipango hiyo ya pamoja.
Kunapotokea kuwa kila mmoja ana malengo tofauti basi hata vipaumbele vitakuwa tofauti na hapo ndipo shida zinapoanzia.
7. Uaminifu
Uaminifu katika mahusiaono ni jambo la muhimu sana. Bila uaminifu ni ngumu sana kwa mahusiano yoyote kudumu.
Uaminifu ni kitu ambacho hujengwa kwa muda mrefu na kikipotea ni ngumu sana kukirudisha. Japo inawezekana kujenga upya uaminifu lakini huchukua muda mrefu sana.
8. Wapenzi,Marafiki na Maisha ya Zamani
Mojawapo ya vyanzo vya ugomvi kati ya wapenzi ni wapenzi wa zamani. Mawasiliano ya aina yoyote na wapenzi wa zamani huleta wasiwasi mkubwa kwa mpenzi wa sasa. Ni kitu ambacho wapenzi wawili wanahitaji kuongea na kupanga jinsi ya kuepukana na matatizo ambayo yanaweza kusababishwa na historia zao za maisha.
Kuepukana na hii ni vyema kuvunya uhusiano wa aina yoyote na wapenzi wa zamani labda tu kama wapenzi hao ni wazazi wenza au mnafanya kazi pamoja na ni ngumu kutokuonana au kuwasiliana.
Suala linalofanana na hili ni uhusiano na baadhi ya marafiki wa jinsia moja ambao wanachukuliwa kuwa mfano mbaya na mpenzi wako. Kama haiwezekani kutowasiliana na kuonana na wapenzi wa zamani au marafiki, basi ni vyema wakawa marafiki wa familia nzima na mawasiliano yoyote kati yenu nao yawe wazi pasipo kificho.
9. Watoto
Suala la uleaji na ukuzaji wa watoto linasababisha ugomvi mara nyingi kati ya wazazi. Jinsi gani mtoto avae au shule ipi aende linapelekea wazazi wengi kugombana.
Ni jambo la muhimu sana kukubaliana juu ya mambo ya msingi juu ya malezi ya watoto. Tofauti za wazazi ziangaliwe kwanza vinginevyo zitaingilia malezi ya watoto na kusababisha ugomvi juu yao.
10. Kazi za Nyumbani
Imekuwa kama utamaduni kwa waafrika kuacha kazi nyingi kama si zote za nyumbani kwa mke. Kwa Wanawake ambao wanafanya kazi pia inakuwa ngumu sana. Hili linasababisha pia ugomvi kwa wapenzi nyumbani. Kama nguo ambazo mume anazivaa na kuzichafua tu bila ya kujali kuwa mweza wake ataumia wakati wa usafi na ikiwa yeye mwenyewe hajishughulishi na kufanya baadhi ya kazi za nyumbani ni wazi itasababisha ugomvi.
Ni vyema wanaume kuchukua baadhi ya majukumu nyumbani hata kama kutengeneza bustani au kulisha chakula mifugo.
Faida ya Ugomvi kati ya Mke na Mme Katika Mahusiano
Japokuwa ugomvi ni kitu cha kuepuka,lakini kina uzuri wake katika mahusiaono kama kikichukuliwa vizuri na kutumika kama kioo.
Kama mtu anagombana na mpenzi wake kwa madhumuni ya kuboresha ni kitu kizuri. Hii inaonesha kuwa anahitaji kuwa na wewe na anahitaji amani.
Ugomvi na mifarakano pia inatoa nafasi kwako kujiangalia vizuri na kama kinacholalamikiwa na mwenzio kina ukweli basi ni nafasi ya kujirekebisha.
Ni mategemeo kuwa kuna kipindi ambapo ugomvi utakuwa mkubwa na baadae wapenzi hao wataelewana na kurekebisha mambo yao.
i. Ugomvi Unatoa Nafasi ya Kuongea Mambo Magumu
Wakati mwingine mazungumzo ya kawaida hayatoi nafasi ya wapenzi wawili kusema yale ya ndani na yanayozizonga nafsi zao. Ugomvi hufungua milango ya hisia za ndani na huenda vyanzo vya matatizo vikawekwa wazi na hivyo kufanyiwa kazi.
ii. Ugomvi unaonyesha Kuwa Mnajali na Mnataka Maboresho
Katika uhusiano ambao wenza hawajali,au hawana malengo ya muda mrefu huwa hawatoi duku zao juu ya utofauti na wapenzi wao.Hivyo wapenzi wanaogombana wanaonesha kuwa wana nia ya dhati na mwenzao na sio tu kupitisha muda.
iii. Ugomvi Unaboresha Uhusiano
Kwa muwa ugomvi unaibua hisia zilizojificha toka kwa wapenzi,ni wakati mzuri kuona matatizo ya kila mmoja. Na kama wapenzi hao wana nia ya dhati ya kuwa pamoja basi watafanyia kazi tofauti na mataizo waliyonayo. Hivyo kuboresha mahusiano yao
Kuna sababu nyingine nyingi ambazo zinachangia ugomvi kati ya mke na mme katika mahusiano lakini haya ni yale yanayotokea katika mahusiano mengi.
Je wewe unasababu nyingine inayosababisha ugomvi na mwenza wako? Shiriki nasi na tuandikie katika sanduku la maoni.
Nawatakia mahusiano mema na wapenzi wenu
No comments