SABABU ZA KUCHOKANA MAPEMA KWENYE NDOA / MAHUSIANO



1)    Kuzoeana

 kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla. Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini. Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau.

2)    Mazungumzo:
 Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake. Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote. Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.

3)     Kusomana Tabia:
 ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa ambao wana mwaka mmoja katika ndoa yao wakawa bado hawajasomana tabia, au wakawa wameishasomana tabia, lakini kila mmoja akawa anataka tabia zake ndio ziwe dira. Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano, aidha hutafuta fursa muafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo yeye haridhiki nayo. Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha.
 4)  Kutamka na kudhihirisha mapenzi:
 Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi wowote, kwa mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna athari nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama. 
 5)   Kupeana zawadi:
 Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako  na nafasi ya mwenzako katika maisha yako, na zawadi ambayo mtu huitoa kwa mwenzake bila ya utangulizi au mnasaba maalum huleta athari njema na huimarisha mapenzi.Na katika zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa, na iwe ni zawadi maalum kwa mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano, si vema kwa mwanamme kumletea mkewe zawadi ya sufuria, microwave, pazia, Dinner set, hiyo haitaitwa zawadi, lakini ni juu yake kumletea manukato ayapandayo, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mumewe achunge vigezo hivyo.
 6)  Kualikana vyakula
Inaweza kushangaza kuwa vipi wanandoa wataalikana chakula wakati wenyewe ni mume na mke, na ni lazima wale pamoja?! Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili mazingira na kufanya vitu makhsusi kwa kushtukizana, huwafanya wanandoa  kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku humfanya mtu kuyachoka, ni vema wanandoa na hasa mwanamke kuwa mbunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyo tia ladha mpya katika nyumba, njia  mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula maalum mumewe peke yake, na hata kama itamlazimu kununua au kuagiza aina tofauti ya chakula basi afanye hivyo, na ampe mwaliko mumewe wa kutokosa kuhudhuria katika mnasaba huo. Aidha mwanamume naye anaweza kumualika mkewe katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliopita.
 7-    Kubadilisha mpangilio wa nyumba: Wanawake wengi huwalalamikia waume zao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala yake kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao. Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba. 
  
8-    Usafi wa mwili na mavazi:
Moja miongoni mwa mambo yanayokera kwa wanandoa ni uchafu wa mmoja wao, uchafu ni sifa isiyovumilika hususan kwa mwanamke, baadhi ya wanawake hudhani kuwa manukato, vipodozi ndio usafi, utakuta anapitisha masiku bila kuoga kikamilifu, bali anapitisha pitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani, kisha kujijaza manukato, lotion na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi na mumewe harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya, hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mkewe, atakaa nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mke huyu. Wanaume nao hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu, kwa mfano wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu, huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi, aidha baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao, na jinsi wanavyojiweka, jambo ambalo linaweza kumsababishia mke maudhi, na hata kujihisi aibu kunasibishwa na mume wake.

No comments