SHOGA, MWILI NI RASILIMALI, UTUMIE KWA FAIDA
Najua nikisema sana nitaonekana kuwa nina mdomo wakati kila kiumbe hapa duniani kina mdomo, lakini kwa vile kuwapasha ndiyo ‘hobi’ yangu acha niwachane live, simuogopi mtu.
Kwa mtindo huu wanawake wachache watabakia katika ndoa zao. Mkisema nachonga sana, sasa sijui nachonga sturi au meza, hivi kweli wewe mwanamke unamwachia mumeo na mikucha na minywele kibao hutaki kumnyoa mpaka aende nyumba ndogo? Aaah! Sipendi miye, hebu mtunze mumeo apendeze, huyo anayetaka kukuibia akose kazi ya kufanya.
Siyo akidondokea nyumba ndogo utasikia jamani kweli mkeo hakupendi hata kucha, huku Ikulu nako kama kichaka cha vibaka kukabia wapiti njia!
Hebu basi tunapowafanyia usafi waume zetu tusiishie kufua tu, bali ni kumfanyia kila kitu kuanzia kucha hadi kumnyoa kila kona ya mwili wake.
Unataka nani aguse mali zako jamani! Mdudu wa sikio hapendi rafiki, kwa kuamini moyo una nafasi moja ya upendo, wengine mnakuwa matawi lakini shina huwa moja.
Usifikirie namaliza nilikuwa naosha mdomo, sasa ndiyo kazi kamili, leo nimekuja na makavu kwa shoga zangu wanaotumia umaarufu wao kuwa na utitiri wa wanaume.
Kwa kweli asiyejifahamu hatajifahamu milele. Kumekuwa na tabia ambayo kila mmoja anakuwa na rundo la wapenzi kwa kuamini yeye ni staa.
Ni jambo lililo wazi sasa hivi kila mwenye jina amezungukwa na watu watano.
Kwa mtindo huu inaonesha wazi kabisa hakuna uaminifu zaidi ya kukidhi haja na tamaa ya mwili. Mtu unapokuwa maarufu kutokana na kuwa staa katika filamu, muziki, mpira na kitu chochote kinachokutangaza kwa jamii, lazima utaandamwa na wapenzi wengi.
Na siku zote kila anayekufuata lazima atakuwa amejiandaa katika ushawishi wa kukuteka kwa kutanguliza fedha mbele.
Shoga, sasa hivi mnaojiita mastaa mmekosa haya wala kujua vibaya, wengi wenu hamjui kusema sitaki kwa kuamini umaarufu haurudii mara mbili, hivyo kila kukicha mnaongeza wapenzi. Jamani hivi umaarufu ni nini? Nakuuliza wewe uliyenitolea macho.
Najua unanilaani kimoyomoyo kwamba naingilia mambo yako, hapo ulipo una ahadi za watu zaidi ya wanne na wote umepanga kukutana nao kila mmoja kwa muda wake. Unaweza kufanikiwa kukutana nao lakini mwisho wa siku utakuwa umepoteza hadhi yako na kukosa wa kukufuata.
Jamani Mungu si mjinga kukupatia umaarufu lengo lake si kukuongezea utitiri wa wapenzi bali kukupunguzia ugumu wa maisha.
Utamsikia mtu, eti siolewi sasa hivi bado nakula maisha. Nani alikudanganya maisha yanaliwa? Maisha yapo kila siku, ila wewe ndiye unayeliwa na maisha ukiisha muda wako unabakia na simulizi mdomoni, kwamba zamani ulipanga wanaume mistari mitatu kama wapiga kura, lakini leo hii umechoka kama paka aliyetumbukia kwenye shimo lenye tope.
Shoga kijua ndicho hiki, usipouanika mkavu utautwanga mbichi, mara nyingi unapokuwa na watu wengi huku ukiwa na mpenzi wako anayejulikana, basi ujue unajiumiza mwenyewe kwani iko siku huyo unayemuona wako atakushitukia na kukuona huna maana.
Penzi halina siri, lazima mmoja wa wapenzi wako atajitokeza mbele ya huyo wako, hapo ndipo utakapokuja juu na kuona umechafuliwa pengine mlikuwa katika hatua za uchumba, hivyo itakuwa imekula kwako.
Wakati unajaribu kukanusha kuhusu huyo mwanaume ghafla anajitokeza mwingine na kusema wewe ni mpenzi wake, utakanusha kwa wangapi? Unaweza kutamani ardhi ipasuke ili ujiingize, je akijitokeza mwingine?
Kutokana na kutojitambua kwako mwanaume wako anaweza asikuamini tena, unampoteza mchumba ambaye labda mlikuwa na malengo mazuri naye.
Napenda kumalizia kwa kuwakumbusha kuwa umaarufu ni maji ya moto, wakati yanachemka ni wakati wako kujipanga kimaisha na si muda wa kuugawa mwili wako kama peremende.
Kumbuka kabla yako kulikuwa na watu maarufu lakini leo hawana thamani tena mbele ya macho ya watu.
Wengi hushindwa kutofautisha kati ya umaarufu na mapenzi, umaarufu hauambatani na mapenzi, kila kitu kinajitegemea, umaarufu humsaidia mtu kufikia malengo yake kwa urahisi na si vinginevyo.
Kwa leo inatosha, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.
No comments