SIKU YAKO IMEKUWA MBAYA ZAIDI??????? FANYA HAYA



Tunaamini kabisa kwamba siyo siku zote huwa zinafanana. Mara nyingine siku huanza vema na kuendelea kwa furaha amani na mafanikio hadi mwisho wa siku hiyo.

Mara nyingine siku yako huanza vibaya na kuishia vizuri, lakini ziko siku ambazo huonekana kuanza kwa mabalaa kama vile bahati mbaya, kupoteza vitu, kuumia, au huzuni ya moyoni na wengine hutabiri muonekano wa siku nzima kuanzia kwa yale yaliyojiri asubuhi. Waswahili wamesema: “siku njema, huonekana asubuhi” maana yake, mara nyingine hata siku mbaya pia hujionyesha katika mwanzo wa siku hiyo.

Najua kuna baadhi ya imani zisizo rasmi ambazo hujaribu kulielezea suala hili. Mfano; Ukiona bundi asubuhi au ukipishana na vyoka njiani basi kuna walakini na siku yako hiyo. Wapo wengine hasa wazungu ambao husema : “ameamkia upande mbaya wa kitanda” sina uhakika kama kuna upande mbaya na mzuri wa kitanda. 


Nia yangu ni kujaribu kukupa namna za kitaalamu zinazoweza kukusaidia kuigeuza siku yako iliyoonekana kuanza vibaya kuwa nzuri na kupunguza pia uwezekano wa kuwepo kwa hizi siku zinazoaminiwa kuwa mbaya.

Maswali
 

  • Je, umewahi kukatishwa tamaa na kitu chochote mwanzoni mwa siku?
     
  • Je, umewahi kupoteza kitu mwanzoni mwa siku?
     
  • Je, umewahi kuumia moyo kwa kupata matarajio hewa (disappointment) mwazoni mwa siku au katika siku fulani?

    Je, umeshawahi kufanya kitu fulani na baadaye ukajutia kukifanya kitu hicho?
     
  • Umeshawahi kufanya kitu na ukajihisi kushindwa au kuaibika?
     
  • Umeshawahi kudhamiria kuingia kwenye uhusinao kwa matumaini yote na mara ukaona kila kitu kina kuwa ndivyo sivyo?
     
  • Au umeshapitia matatizo fulani ya mwili, kama vile Ugonjwa, ukilema na ukaona labda ndiyo chanzo cha ugumu wa maisha yako?

Kama wewe ni mmoja wa watu hao basi karibu katika ulimwengu wa wanadamu wa kawaida, namaanisha hayo ni mambo ya kawaida kabisa kwa mtu wa kawaida. Wakati tunaposhindwa, au kujihisi tumeshindwa mara nyingi tunadhani sisi peke yetu ndiyo tu wenye hali hiyo, ukweli ni kwamba, wengi hupitia huko na yamkini katika hali ngumu zaidi. 


Kila mmoja wetu amewahi kushindwa katika kitu fulani. Kila mmoja wetu amewahi kujutia jambo fulani alilolifanya, kila mmoja wetu amewahi kukutana na magumu.

Mambo ya kuzingatia:
 

Jikubali kama mwanadamu wa kawaida na kwamba haistajabishi kushindwa
 

Yamkini unakata tamaa maana umezungumza na watu wanaoshinda na kufanikiwa tu, angalia upande wa pili, zungumza pia na waliowahi kushindwa.
 

Haijalishi ni muda gani, ni kiasi gani, ni ukubwa gani, ni uzito kiasi gani, wa magumu uliyopitia ninachojua ni kwamba inawezekana mimi na wewe kunyanyuka tena toka kushindwa kwetu, ndoto zetu zaweza kuwa kweli tena. Hii inategemea na kiasi cha uvumilivu wako.

Tatizo siyo kushindwa. Kushindwa kwa ukweli ni kule kushidwa kunyanyuka tena mara baada ya kushindwa mara ya kwanza
Angalia mchezo wa ngumi, haijalishi mtu anapigwa na kuanguka mara nyingi kiasi gani, lakini pale anaposhindwa kunyanyuka ndiyo refa hutangaza “KNOCK OUT” yaani ameshindwa kabisa.

Ili kuweza kunyanyuka tena;
 

Jikubali kama mwanadamu wa kawaida tambua kushindwa kupo na ni moja ya matukio ya maisha yetu.
 

Unapoanguka chini, jitahidi usibaki chini. (Tofautisha kuanguka kwa mtoto na mtu mzima) fahamu kushindwa kwa kweli ni kule kushindwa kunyanyuka mara baada ya kuanguka.

Jifunze, pata shule kupitia mapito na magumu unayoyapitia, tatizo pia siyo kufeli, bali ni kufeli kujifunza katika kule kufeli. Kufanye kushindwa kwako kuwe kama mawe ya kukanyagia katika kuvukia kwenda upande wa pili.

Tutakushangaa, ukiangushwa na jambo lile lile linalokuangusha mara zote.


Jifunze kutumainia katika imani uliyonayo. Imani ni injini isiyoshindwa. katika suala zima la kushindwa na kuweza. Imani huwa poozeo kwa maumivu tunayoyapitia.

Jitahidi, vuta zaidi, kazana, amini kuwa kitu chema chaweza kutoka katika mikono yako, midomo yako, moyo wako au hata mawazo yako.

No comments