Je Wajua Kwanini Wanawake Hula Vyakula vya Ajabu Ajabu Wakiwa Wajawazito?
Tabia hii inayojulikana kwa Kiingereza kama “Pica” inatokana na mtu
kutamani kula vitu vyenye virutubisho kidogo sana au visivyo na
virutubisho vya aina yoyote kwa mwili.
Tamaa hizi huwa zinawapata watoto au mama mjamzito kutafuna vitu ambavyo
kimsingi si chakula – kama udongo au chaki. Jina hili la pica ni aina
ya ndege ambaye anajulikana kwakuwa anakula kitu chochote, hana
anachochagua. Ni kweli kwamba wajawazito wengi hupata hamu ya kula vitu
ambavyo si vyakula walivyozoea kula mara kwa mara wakiwa si wajawazito;
wengi wao ni rahisi kuwaelewa kwa sababu hukimbilia mchele, barafu na
vinginevyo ambavyo si vitu vibaya kula.
Kwa watoto, hii ni tabia iliyozoelekakwakuwa inawatokea watoto wengi
ambao ni kati ya asilimia 25 na 30% ya watoto wote; lakini kwa wanawake
wajawazito, inatakiwa iwe kwa kiwango cha chini zaidi.
Nini kinasababisha tabia hii kwa wajawazito?
Sababu ya baadhi ya wanawake kuwa na tabia hii wakati wa ujauzito
haijulikani hasa. Kwa sasa hakuna sababu maalumu, lakini kwa mujibu wa
Jarida la Chama cha Watu Wanaoishi na Ugonjwa wa Kisukari nchini
Marekani, tabia hii yawezekana ikasababishwa na upungufu wa madini ya
chuma mwilini. Baadhi wanadai kwamba hali hii inaashiria kwamba mwili
unajaribu kupata vitamini na madini mengine yanayokosekana kwenye
chakula cha kawaida ambacho mtu anakula. Muda wingine tabia hii
yawezaikatokana na kuumwa viungo au akili kwa muda mrefu.
Baadhi ya vitu vya ajabu ambavyo wajawazito hupenda kula
Vitu vinavyopendwa zaidi na wajawazito wengi ni udongo, uchafu. Vitu
vingine ni njiti za kiberiti zilizochomwa, mawe, mkaa, barafu, dawa ya
meno, sabuni na mchanga. Mjamzito anapokula vitu hivi hujisikii raha
kana kwamba amekula chakula chenye faida kubwa kwake na kwa mtoto aliye
tumboni.
Kuna hatari yoyote kwa mtoto aliye tumboni?
Kula vitu ambavyo si vyakula kimsingi ni jambo linaloweza kusababisha
madhara kwa mjamzito mwenyewe na mtoto aliye tumboni. Kula vitu hivi
kunaweza kuharibu mfumo wa kawaida wa kunyonya virutubisho kutoka kwenye
vyakula na kusababisha mwili wako upungukiwe na madini muhimu
unayoyahitaji kwa afya yako na ya ukuaji wa mtoto vilevile. Tabia hii ni
hatarishi sana kwakuwa vitu ambavyo si vyakula vinaweza kuwa na
viambata ambavyo ni sumu au vyenye vijidudu vinavyoathiri mwili.
Kudhibiti tabia hii
Usihamaki unapojikuta unatamani vitu vya ajabu ajabu wakati wa ujauzito:
inatokea sana na si jambo la kushangaza kwako pia. Jambo la muhimu ni
kumjulisha muuguzi wako au wahudumu wa kliniki unayohudhuria kujua
maendeleo yako ya mtoto tumboni ili akuelimishe na ahakikishe kwamba una
uelewa kuhusu hatari zinazoambatana na tabia hiyo.
Baadhi ya mbinu za kutumia kushinda tamaa hizo
- Mtaarifu mhudumu wako wa afya kwenye kliniki unayohudhuria na muangalie kumbukumbu za ukuaji wa mtoto tumboni pamoja na hali yako ya kiafya
- Fatilia kiwango chako cha madini ya chuma mwilini pamoja na kiwango cha vitamini na madini mengine unayotakiwa kula
- Omba ushauri kuhusu kitu gani uwe unakula ili kubadili ili kuepuka vitu vya ajabu (waweza kumung’unya/ kutafuna vitu kama pipi au ‘big g’ isiyo na sukari
- Mwambie hata rafiki yako mmoja kuhusu hamu hizi na umtake awe anakukataza unapokula vitu vya ajabu
No comments