Kukabiliana na Hasira Ambayo Inaweza Kusababisha Matatizo.



Hasira ni kama gharika inayoanzia kwenye ufahamu wako. Unapohisi imekuja unatakiwa uelekeze mawazo yako kwenye pumzi. Yenyewe itaanza kubadilika na mtazamo wako juu yake utabadilika - Thich Nhat Hanh.
Ulishawahi kukutana na watu wenye hasira muda wote? Wao muda mwingi wanautumia kutumia sauti kubwa katika kuelekeza watu na muda mwingine hawapatani na watu wengi? Wengine wanaamini kuwa hasira ni asili ya mtu lakini mimi naamini hasira ni udhaifu ambao tunajizoesha wenyewe na hatimaye tunashindwa kujiongoza kwa hilo. Kuna wakati hasira inaweza kukutawala na ukashindwa hata kujijua na ukaja kutambua kuwa ulikuwa na hasira baada ya matokeo. Wengine wanajiua, wanadhuru watu, wanaharibu vitu, na mpaka wengine afya yao inabadilika kutokana na hasira wanayoishikilia. Kuna msemo mmoja niliwahi kuusema katika Blogg hii kwenye mada ya aina za watu kutokana na hasira zao nilisema kuwa
Hasira ni kama kaa la moto, unapolishikilia kwa lengo la kumdhuru mwenzio unajiunguza na wewe pia.
Unapoweka hasira akilini unajikosesha raha, sio kwamba kila mwanadamu hana hasira, bali wanadamu tunatofautiana jinsi tunavyotenda kutokana na hasira. Hasira inaweza kukujia lakini ukaweka akili na fikra yako katika mawazo mengine chanya na taaratibu akili itaama kutoka kwenye hasira na utakuwa huru nayo.
Itazame kwanza hasira yako na jaribu kuichunguza imetokana na nini.

Kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kupelekea hasira, mfano mtu amekutendea kitendo ambacho hujakipenda, Mara nyingi hasira hutokana na hali au kitendo ambacho kimeenda kinyume na tunavyopenda au tunavyotegemea. Kuna wakati hasira inaweza kuwa imetokana na wasiwasi, na hapa ndipo unatakiwa uchunguze hasira uliyonayo imetokana na nini? Je imetokana na asili yangu ya kuwa na hasira kila wakati au? Je imetokana na wasiwasi? Je kinachosababisha niwe na hasira ni cha kweli au ni wasiwasi wangu tu? Je kuna mazoea ambayo nimejiwekea ambayo yanapelekea hasira hii? Ni vyema kufahamu hayo kwani unaweza kukuta hasira uliyonayo imetokana na hisia tu na sio uhalisia. Unaweza ukachunguza na kufahamu kuwa kumbe ilikuwa haina haja ya kuwa na hasira.

Tambua kuwa hasira haimuumizi tu mtu anayeishikilia bali mpaka na maisha yake.

Kuna watu wao wameshajichukulia kuwa hasira ni hasira tu. Wao hasira ikiwatokea wanajisahau na kuanza kutenda mabaya kama vile kulipiza kisasi kwa waliomkosea, kuvunja vitu na wingine wanafikia hatua ya kujiuza kabisa. Ni vyema kufahamu kuwa hasira ikizidi ni mbaya sana.
Pia kuishikilia hasira unajinyima raha na uhuru, unaanza kutumia muda wako kuwaza badala ya kuutumia muda wako kufurahia uhai wako na kushukuru kwa kila jambo.
Hasira ikikuanza, ipe muda kwanza kabla ya kufanya maamuzi.

Pale hasira inapokutokea ni vyema kutokuwa mwepesi kuisikiliza hasira yako. Hasira muda wote huja na jibu au tendo linalokushawishi ulitende. Mara nyingi jinsi hasira inavyochemka na maamuzi yake nayo yanakuwa mabaya na hasira inapopoa uamuzi wake angalau unakuwa sio mbaya sana. Kama hasira ikikuanza na ukaona unaweza kufanya maamuzi mabaya ni vyema kuipa muda, usikubali kufanya maamuzi ya haraka. Itakusaidia kutafakari kwa kina na labda kama kuna kitu ulikuwa haukifahamu kinaweza kujidhihirisha na kuweza kufanya hitimisho sahihi.

Jifunze kukubaliana na hali.

Wengi ambao ni wagumu sana kukubaliana na hali ni wepesi sana kuwa na hasira. Kuna wakati hasira hutokana na mategemea, unategemea tokeo fulani au kitu fulani halafu mambo yanakuwa tofauti. Hasira inakushawishi usikubali, na jinsi unavyozidi kutokukubaliana na hali ndipo unazidi kuwa mtumwa wa hasira yako. Kuna hali ambazo hasira ikikujia, ukiamua kukubaliana na hali na hasira nayo inaondoka. Wengi wanashikilia vitu, umaarufu, mali, sifa, n.k na kushindwa kuviachia. Jifunze kuacha mambo yaende kama yalivyo Jifunze kukubaliana na maisha katika hali zozote. Kubali kuwa hujaja na chochote hapa duniani na hutaondoka na chochote, jiweke huru kwa lolote. Utaona maajabu yake pale utakapoamua kuishi kama mtoto mdogo asiye na hasira kwani ni mwepesi kukubaliana na hali, atalia tu akiona hali sio nzuri kwake lakini baada ya muda anasahau.

Jifunze meditation na kutazama pumzi.

Kila wakati na hata hapa ulipo unapumua, lakini ni mara chache sana katika maisha yako umeweza kuweka akili yako kwenye pumzi yako. Unapoweka akili kwenye pumzi unapunguza mawazo yaliyo kwenywe akili. Akili muda wote inashikiliwa na mawazo, akili inayoshikiliwa na mawazo muda wote ni taabu sana kuiongoza, inakuwa rahisi kushikiliwa na mawazo, hisia na hasira. Unapojifunza kuweka akili yako kwenye pumzi, unapohesabu pumzi inayoingia na kutoka taaratibu, unapoweka akili yako sehemu moja unapunguza mawazo mengine ambayo yanazunguka kichwani na kukufanya uwe huru kwa kuwa na mawazo machache.
Sawasawa na meditation, ukiweza kutafuta muda wa kumeditate utajikuta unakuwa mzuri katika kufanya maamuzi na kuwa na furaha na kukubaliana na changamoto

No comments