OOH MY STORY! (Mkasa wa Kweli) "MKE WANGU, WEWE NI KATILI SANA! SITAKUSAHAU!"
Mwandishi: Hashim Aziz (Hash Power)
@Daktari Wa Mapenzitz
Jina langu naitwa Judcket, napenda kuwashirikisha juu ya mkasa ulionitokea kwenye maisha yangu, ukimhusisha mke wangu ambaye kwa sababu maalum naomba nisimtaje jina lake.
Historia yangu kwa kifupi, mimi ni mzaliwa wa Machame, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. Licha ya kwamba nimezaliwa Kilimanjaro, maisha yangu mengi nimeishi jijini Arusha. Nimezaliwa katika familia ya watoto sita, mimi ni mtoto wa tatu, baba yetu alikuwa ni daktari na mama alikuwa ni mama wa nyumbani.
Tofauti na wenzangu kwenye familia yetu, mimi sikupata bahati ya kusoma, nilipohitimu darasa la saba tu, nilienda Arusha kwa ndugu yangu ambako baadaye nilijifunza ufundi umeme. Namshukuru Mungu kwani kazi yangu ya ufundi iliweza kunipatia madili mengi kwa haraka.
Nikawa nasafiri kwenda sehemu mbalimbali, nimeshafanya kazi kwenye machimbo ya Mererani na baadaye nilipata dili kubwa kwenye ujenzi wa hoteli za kitalii kwenye mbuga za wanyama za serengeti.
Kazi niliyokuwa nafanya Serengeti, naweza kusema ndiyo iliyoyabadilisha maisha yangu kwani niliweza kuhama pale kwa ndugu yangu nilipokuwa naishi na kupanga chumba changu mwenyewe.
Nikaanza kununua vitu mbalimbali vya ndani, kiufupi nilijikamilisha kimaisha. Ikawa siku za mapumziko narudi kwangu, nakaa Arusha na siku za kazi naenda Serengeti. Unajua tena maisha ya ujana, katika kipindi hicho nilikutana na dada ambaye nilianzisha naye uhusiano wa kimapenzi.
Ulikuwa ni urafiki wa kawaida wa mtu na mpenzi wake, yeye alikuwa akifanya kazi kwenye mgahawa mmoja kwenye Soko Kuu la Arusha, mahali nilipokuwa napenda kwenda kula chakula, si unajua kipindi hicho nilikuwa bado naishi kibachela kwa hiyo chakula nilikuwa nakula mgahawani.
Uhusiano uliendelea kushamiri lakini kiukweli hatukuwa na malengo yoyote kwa kipindi hicho. Baadaye, yule dada akaja kunasa ujauzito wangu, jambo ambalo kimsingi lilinichanganya sana kwa sababu kwanza nilikuwa sijajipanga kupata mtoto wala kuoa kwa kipindi hicho.
Baada ya mama yake kujua kwamba amepata ujauzito, kwa sababu alikuwa ananijua na alikuwa anaujua uhusiano wetu, aliniita na kuniweka chini, akaniambia haiwezekani nimharibie binti yake maisha halafu nikatae kumuoa, akaniambia hataki kumuona nyumbani kwake, nitajua mwenyewe cha kufanya.
Akamfukuza nyumbani kwake ambapo alipokuja kwangu, nilimwambia hakuna namna, inabidi tuishi tu pamoja wakati akiendelea kujisikilizia hali yake. Baadaye, sikuwa na ujanja, ikabidi nikamtambulishe nyumbani kwa wazazi wangu.
Nakumbuka baba yangu aligomba sana, akaniambia kwamba kwa nini nakimbilia kuoa wakati sikuwa nimejiandaa? Isitoshe kaka zangu walikuwa wakubwa lakini bado hawakuwa wameoa, akaniuliza naharikishia nini? Kimsingi familia haikuafiki lakini sikuwa na namna, tukarudi Arusha ambapo tuliendelea na maisha.
Baadaye alijifungua mtoto wetu wa kwanza, kipindi hicho bado nilikuwa naendelea na kazi kwa hiyo maisha hayakuwa yakinisumbua sana. Baadaye tulishauriana na mwenzangu kwamba nimfungulie biashara kwa sababu mtoto alishachangamka.
Kweli nilimpa msingi, akawa ananunua magunia ya karoti na kwenda kuyauza sokoni, namsifu sana kwa sababu alikuwa ni mchakarikaji sana kwenye kutafuta fedha. Bado ndugu zangu walikuwa hawajamkubali lakini kwa sababu ndiyo niliyekuwa naishi naye na tayari tulikuwa na mtoto, hawakuwa na cha kufanya.
Changamoto ndogondogo zilikuwepo, unajua tena hamuwezi kuishi watu wawili pamoja halafu mikwaruzano ikakosekana lakini tulikuwa tukiyamaliza, wakati mwingine mama yake ndiye aliyekuwa akitusuluhisha kwa sababu tulikuwa tukiishi jirani naye.
Maisha yaliendelea, akapata ujauzito wa pili na baadaye akajifungua salama, miaka ikaendelea kukatika na hatimaye akapata ujauzito wa tatu. Kwa kipindi chote hicho, japokuwa sikuwa nimemuoa lakini tulikuwa tukiishi kama mume na mke na hata watu wote walikuwa wanajua sisi ni mume na mke halali.
Maisha yalianza kuyumba baada ya mkataba wa kujenga hoteli kule Serengeti kufikia mwisho, nikarudi mtaani nikiwa sina kazi, biashara yake ndiyo ikawa inaendesha familia yetu. Narudia tena kusema mwenzangu alikuwa mchakarikaji sana, kwa hilo nampongeza.
Baada ya kukaa bila kazi kwa muda mrefu, niliwasiliana na kaka yangu aliyekuwa akiishi jijini Dar es Salaam, akaniambia amenitafutia kazi kwenye kampuni moja kwa hiyo nije Dar lakini akanipa masharti kwamba kwa sababu kazi yenyewe haikuwa ya uhakika na ndiyo kwanza nilikuwa naanza, niiache familia Arusha nije Dar peke yangu.
Baada ya kujadiliana sana na mke wangu, kweli tulikubaliana nifunge safari, nikamuahidi kwamba mambo yakiwa mazuri nitaenda kumchukua. Nakumbuka niliingia Dar es Salaam ilikuwa ni mwaka 2010, karibu na kipindi cha uchaguzi, nikafikia nyumbani kwa kaka maeneo ya Jet, Kipawa.
Kweli baada tu ya kufika, alinitafutia kazi kwenye Kiwanda cha Korie kilichokuwa hukohuko Kipawa, nikaanza kazi nikiwa kama fundi umeme.
Kiukweli ujira niliokuwa nikipata ulikuwa mdogo sana kwa sababu nilianza kama kibarua lakini namshukuru kaka yangu aliniambia kuwa fedha ninayopata inisaidie kwa mambo yangu binafsi tu lakini kuhusumambo ya chakula na sehemu ya kulala, yeye ndiyo atakuwa anasimamia kila kitu.
Kweli niliendelea na kazi, nikawa fedha ninazopata nakusanya na kumtumia mama watoto wangu ambaye naye kule Arusha alikuwa akiendelea kuhangaika na biashara. Siku zilizidi kukatika na hatimaye mwaka mmoja ukawa umeisha.
Japokuwa nilikuwa napata kila kitu nyumbani kwa kaka yangu, lakini binafsi sikuwa huru kwa sababu ya kuwa chini ya usimamizi wa mtu fulani wakati huko nilikotoka nilizoea mimi kuwa ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho.
Kutokana na fedha nilizokuwa naweka, niliweza kupata za kutosha kununua kitanda na godoro pamoja na za kulipia kodi ya miezi sita. Nilifanya mambo yote kimyakimya kwa sababu siku zote kaka alikuwa ananiambia bado sijaweza kusimama na kuendesha maisha mwenyewe jijini Dar es Salaam, akanitaka niendele kujipanga zaidi.
Licha ya upendo aliokuwa akinionesha, ilibidi tu nimwambie ukweli kwamba nashukuru kwa msaada wake lakini siwezi kuendelea kukaa kwake, nikamwambia ukweli kwamba tayari nimeshapanga chumba na kupata msingi wa kuanzia hivyo nataka nikaishi mwenyewe.
Alinikubalia kwa shingo upande, akaniambia anajua nimefanya hivyo kwa sababu nataka kumleta mama watoto wangu, akanionya kwamba nikimleta wakati bado maisha sijayamudu atanisumbua kwa hiyo ni bora niwe na subira, nikamuitikia tu lakini moyoni nilishaamua uamuzi wangu.
Kwelisikukadhaa baadaye nilimpigia simu mama watoto wangu, nikwambia kwamba nimeshapata chumba na namuomba aje Dar es Salaam tuendelee kuishi pamoja, akafurahi sana kusikia hivyo.
Nilimwambia kwa sababu ndiyo kwanza nayaanza maisha na nimepanga chumba kimoja tu, aje yeye peke yake, watoto awaache kwa bibi yao na achukue vitu vichache kama TV na nguo tu. Nikamtumia naulina kweli siku chache baadaye, nilienda kumpokea na kwenda mpaka Mtaa wa Msimbazi, hukohuko Kipawa nilikokuwa nimepanga chumba.
Alifurahi sana kwa sababu ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika Dar, akanishangaa kwa sababu nilikuwa nimekonda sana tofauti na wakati niko Arusha, nikamwambia ni kwa sababu ya ugumu wa maisha na mawazo juu ya familia yangu, akaniambia nisijali kwani yeye yupo.
Nikama alikuja na baraka zake kwani siku chache baadaye, kazini ambako nilikuwa nikifanya kazi siku zote kama kibarua, nilipewa mkataba wa mwaka mmoja ambao sasa ulimaanisha kwamba hata malipo yangu yatakuwa mazuri. Tulifurahi sana kwa pamoja, tukayaanza maisha mapya.
Kiukweli mapenzi yetu yalikuwa matamu mno, ilikuwa kama ndiyo tumetongozana na kuyaanza maisha mapya, tulipendana, tulisikilizana na kuelewana sana, yaani kila mmoja alikuwa akituonea wivu. Hata mke wangu naye alibadilika sana kitabia, akawa ananionesha mapenzi ya dhati ambayo yalinifanya nizidi kumpenda.
Sikuzilizidi kusonga mbele, nikampeleka kwa kaka kumtambulisha ambaye alifurahi ingawa bado alionesha kuwa na wasiwasi kama kweli nitaweza kumudu familia jijini Dar. Kwa kuwa mke wangu alikuwa amezoea kujishughulisha, aliniambia anajisikia vibaya kukaa nyumbani tu,akaniomba nimpe msingi ili na yeye aanze kujishughulisha tusaidiane kuendesha familia.
Kwelinilimkubalia, kuna mchezonilikuwa nacheza pale kazini, nilipopokea nikamchukua mpaka Kariakoo, nakumbuka ndiyo ilikuwa siku yake kwanza kufika Kariakoo, nikamnunulia friji dogo, ‘blender’ ya kutengenezea juisi na vifaa vingine, fedha iliyobakinikamfanyia ‘shopping’ ya vitu vyake binafsi.
Bado alikuwa hajaelewa malengo yangu yalikuwa nini, tulipofika nyumbani nikamwambia kwamba nataka aanze kutengeneza juisi mimi nitamtafutia soko. Nilipanga kwamba awe anakuja kuuzia palepale kazini kwetu kwa sababu kulikuwa na wafanyakazi wengi ambao wangeweza kuwa wateja wazuri wa juisi.
Kweli siku chache baadaye mke wangu alianza kutengeneza juisi, akawa analeta pale kazini. Nikamtafutia wateja na kiukweli kwa sababu ya ubora wa juisi yenyewe, ndani ya mudamfupi tu alipata wateja wengi, mpaka Wahindi wakawa wanakunywa juisi yake, akawa anaingiza fedha nyingi sana kwa siku.
Maisha yajazidi kutunyookea, tukapanga nyumba kubwa zaidi na kwa sababu sasa tulikuwa tukijimudu, tulikubaliana kwamba aende kuwachukua watoto. Kweli alifanya hivyo, akaenda kuwachukua watoto lakini tofauti na makubaliano, alienda kumchukua na ndugu yake mmoja wa kike kwa madai kwamba anataka awe anasaidiana naye kwenye biashara hiyo.
Sikuwa na kipingamizi, akaja naye na maisha yakaendelea. Miezi michache baadaye, alienda tena kwao, cha ajabu hakufika kwetu na aliporudi alikuja na ndugu zake wengine watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume, ukichanganya na watoto wetu watatu na yule ndugu yake wa kwanza aliyekuja naye, familia ikawa kubwa sana.
Kibaya zaidi, wale ndugu zake aliokuja nao, wote walianza kwenda kazini eti kumsaidia kuuza juisi lakini hawakuwa wakienda kwa ajili ya kazi hiyo, wakaanza mambo ya wanaume, kazini kwetu wakawa gumzo kubwa kwelikweli, wakawa wanagombanisha wanaume hovyo, lawama zote zikawa zinakuja kwangu.
Ikafika mahali, juisiikawa inatengenezwa vibaya, na wao wakienda kuuza kazi ni kubadilisha wanaume, wateja wakaanza kukimbia huku wengi wakinilaumu sana mimi. Kibaya zaidi, siku chache baadaye mkataba wangu wa kazi uliisha na nikawa sina kazi tena. Hapo ndipo nilipoelewa maana ya ule usemi wa filisika ujue tabia ya mkeo.
Baada ya mkataba kuisha pale kazini, nililipwa stahiki zangu kisha nikarudi nyumbani. Walinipa ‘option’ kama nataka niendelee nakazi basi niwe kibarua lakini mwenyewe nikaona siyo sawa nitoke kuajiriwa hadi kuwa kibarua, ngazi ambayo tayari nilikuwa nimeshaivuka zamani.
Nilichokifanya ilikuwa ni kurudi nyumbani kutuliza kichwa kwa sababu nilishaamua kusonga mbele. Siku za mwanzo mke wangu alificha makucha yake, akawa anaendelea kuihudumia familia yeye kwani misingi ya biashara niliyomjengea ilikuwa ikimuingizia fedha za kutosha kuilisha familia.
Lakini kwa kipindi hicho ikumbukwe kwamba hata kabla sijaachishwa kazi, tayari alishaanza kuonesha dharau kwangu, likiwemo suala la yeye kuwa anasafiri mara kwa mara kwenda kwao Arusha bila kuniaga na kwenda kuwaleta ndugu zake bila idhini yangu.
Kwa jinsi nilivyokuwa namjua mke wangu, nilijua lazima atatumia kigezo cha mimi kutokuwa na kazi kulipiza kisasi kwangu kwa sababu siku za mwanzo nilikuwa na nguvu ya kumwambia hiki sikitaki kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa naendesha familia.
Nilijifikiria kwamba kama katika kipindi ambacho nilikuwa na kazi bado alikuwana uwezo wa kunikosea adabu na kunijibu alivyokuwa akijisikia, itakuwaje sasa hivi sina kazi? Niliamua kumuachia Mungu. Kile nilichokitabiri kilianza kutokea, mke wangu akaanza upya vituko vyake.
Awamu hii, safari za kwenda Arusha kwao zilikuwa haziishi, mara anaondoka wakati mwingine bila hata kuaga, baadaye ukimpigia simu anakwambia niko Arusha kwa mama, ukimuuliza kwa nini hujaniaga, anajibu anavyojisikia yeye.
Kiukweli nilikuwa nikiumia sana moyoni lakini sijui mwenzenu nimeumbwaje? Sina kabisa hulka ya kugombanagombana. Ikawa akirudi anakaa siku mbili tatu anasafiri tena, halafu akienda Arusha anaishia kwao, hata kwetu Moshi hataki kufika japokuwa alikuwa akipafahamu.
Nilijitahidi kumvumilia mke wangu lakini nikaona visa vinazidi kuongezeka, akawa ananijibu vibaya hata mbele ya ndugu zake halafu nakosa cha kuzungumza nabaki na maumivu yangu tu moyoni.
Kiukweli mateso yalizidi, mke wangu akabadilika kabisa, akawa haniheshimu hata chembe na nikimuuliza, ananiambia sina haki ya kuhoji chochote kwa sababu yeye ndiyo alikuwa kama baba wa familia kwa sababu anatulisha wote.
Wale ndugu zake waliokuwa wakiendelea kuuza juisi kule kazini nilikosimamishwa, nao waliendelea na vituko, nikawa napewa tu taarifa za jinsi wanavyoendelea kutia aibu kwa kuchanganyachanganya wanaume kila kukicha.
Ikafika mahali nikawa tena sina kauli, pale nyumbani familia ilikuwa kubwa mno. Pale kulikuwa na wale wasichana wawili alioenda kuwachukua Arusha kwa kisingizio cha kuja kumsaidia biashara, walikuwepo wifi zake wawili, wadogo zake wa kiume wawili na mtoto mmoja wa wifi yake.
Ukichanganya na wanangu watatu, unaona jinsi familia ilivyokuwa kubwa. Kila nilipomshauri kwamba hao ndugu wanapaswa kupungua pale nyumbani kwa sababu tumeyumba kimaisha na inabidi tusimame upya kama familia, yaani mimi, yeye na watoto wetu kwanza halafu mambo yakinyooka ndiyo akawachukue tena ndugu zake, alikuwa hataki kabisa, akawa ananijibu kwamba naumia na nini wakati hao ndugu zake yeye ndiye aliyekuwa akiwalisha?
Kiukweli mateso niliyokuwa nayapata yalinifanya niyakumbuke sana maneno ya kaka yangu siku nilipoenda kumwambia kwamba nahama nyumbani kwake kwa sababu nataka nije kuishi na mke wangu. Ama kweli waliosema asiyesikia la mkuu huvunjika guu hawakukosea, maji yalikuwa yamenifika shingoni.
Nikakonda sana kwa sababu ya mawazo, kaka yangu ambaye alikuwa akijua kila kilichokuwa kinaendelea, alinishauri kama inawezekana nirudi tena kwenye mikono yake huyu mwanamke nimuache aendelee na mambo yake lakini sikukubaliana naye.
Katika kuokoa uhusiano wetu ambao sasa ulikuwa ukiendelea shimoni, nilijaribu kuwashirikisha watu wetu wa karibu, upande wa familia yaani kwao na kwetu, vikao kadhaa vya kutusuluhisha vikafanyika lakini mwenzangu ni kama alishakuwa sikio la kufa, hakusikia chochote na wala hakubadilika.
Uamuzi wa mwisho niliofikia, nikaona ni bora mimi niondoke pale nyumbani kwa sababu sikuwa na msaada tena kwake na hata thamani yangu haikuonekana tena. Nikajaribu kuwashirikisha baadhi ya watu lakini wakaniambia nisikubali mwanamke anitawale, niendelee kupambana naye.
Kama nilivyosema, kihulka mimi siyo mtu wa kushindanashindana, nikaamua kuinua mikono. Kipindi ambacho moyo wangu ulikuwa tayari umeshakinai, akamchukua mtoto wetu mkubwa ambaye sasa yupo kidato cha pili, akamhamishia Arusha bila hata kunishirikisha.
Hatujakaa sawa, akawachukua na wanangu wengine wawili, mmoja anasoma darasa la sita na mwingine la tatu, nao akawarudisha kwa mama yake Arusha, nikaona kweli amedhamiria kunivuruga kichwa changu. Sikumwambia chochote, nilichokifanya ilikuwa ni kutafuta chumba kingine, nikalipa kodi ya miezi sita.
Baada ya kukamilisha mambo yote, nikampa taarifa kwamba kwa jinsi mimi na yeye tunavyoishi, anavyonikosea adabu, asivyotaka kunisikiliza na dharau anazonionesha, nimeamua kwenda kuanza upya maisha yangu mbali na yeye.
Sikutaka kuchukua kitu chochote kutoka pale nyumbani, nilichukua kitanda kimoja tu pamoja na sanduku langu la nguo, nikahamia kwenye chumba nilichopanga na hivi tunavyoongea, tayari nimeyaanza maisha mapya.
Najua nitapata shida kwa muda kwa sababu sina kazi na sijafanikiwa tena kupata lakini naamini ipo siku Mungu atanifungulia tena milango ya riziki, nitapata kazi na huenda nikampata mwanamke mwingine ambaye atanipenda kwa dhati na kukubaliana na hali halisi ya maisha yangu.
Nasikia wale wasichana waliokuwa wakiuza juisi, wote wawili tayari ni wajawazito na huyo mmoja ameshaondoka kwenda Arusha kujifungua. Mambo mengine ni kama Mungu analipa hapahapa duniani. Hayo ndiyo yaliyonitokea lakini bado sitaki kukata tamaa, kila siku namuomba Mungu aweze kunisaidia nisimame tena.
Mwisho.
No comments